Mlinda mlango mpya wa majogoo wa jiji (Liverpool) Alisson Becker anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha klabu hiyo kwa mara ya kwanza mwishoni mwa juma hili, wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya SSC Napoli ya Italia.

Uhakika wa mlinda mlango huyo kukaa langoni kwa mara ya kwanza tangu aliposajiliwa mwezi uliopita akitokea AS Roma ya italia, umetolewa na meneja wa Liverpool Juergen Klopp.

Meneja huyo kutoka nchini Ujerumani amezungumza na mwandishi wa habari wa Tovuti ya Liverpool FC, na kueleza mkakati wake wa kumtumia Alisson katika mchezo huo ambao utakua wa mwisho, kabla ya kuanza kwa mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini England mwishoni mwa juma lijalo.

“Ni wakati mzuri kumtumia kwa mara ya kwanza katika kikosi chetu, tutacheza na SSC Napoli siku ya jumamosi, ninaamini atakua tayari kuonyesha uwezo na umahri wake, mashabiki nao wataona kwa nini tumemsajili Alisson katika kipindi hiki cha kuelekea msimu mpya,” Alisema Klopp

“Amefanya mazoezi ya kutosha tangu alipojiunga na wenzake, ninaamini anatosha kukaa langoni kupitia mchezo dhidi ya SSC Napoli.”

Alisson alianzaa mazoezi na kikosi cha Liverpool mapema juma hili, baada ya kumaliza likizo ya mapumziko, kufuatia jukumu lililomkabili nchini Urusi la kuitumikia timu ya taifa ya Brazil, ambayo iliondolewa katika hatua ya robo fainali kwa kufungwa na Ubelgiji mabao mawili kwa moja.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25, alisajiliwa na Liverpool kwa ada ya uhamisho wa Pauni Euro milioni 72.5 sawa na dola za kimarekani milioni 84, na kuweka rekodi ya kuwa kipa ghali zaidi duniani.

Kikosi cha majogoo wa jiji kitakapomaliza mchezo huo kirafiki dhidi ya SSC Napoli utakaochezwa mjini Torino-Italia Agosti 07, kitarejea nchini England tayari kwa mpambano wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya West Ham United.

Kairuki awatangazia kiama watoroshaji wa Tanzanite
Adhabu ya baba yamuua mwanaye, mahakama yamsweka jela