Sanaa na ubunifu ni muhimu zaidi katika taifa lolote duniani, tasnia hii ndiyo iliyopelekea kupatikana kwa jina la Tanzania, baada ya kuungana kwa nchi mbili huru za Tanganyika na Zanzibar, Aprili 26 mwaka 1964.

Jina hilo la Tanzania lilibuniwa na kijana wa enzi hizo ambaye yuko hai hadi leo akiufaidi uzee wake huku akilisikia jina alilolibuni yeye, Mzee Mohammed Iqbal.

Hivi karibuni, Mzee Iqbal anayeishi zaidi nchini Uingereza, alifanya mahojiano Maalum na kipindi cha Sunrise cha 100.5 Times Fm na kueleza namna alivyoweza kubuni jina hilo pamoja na kiasi alichopewa kama zawadi.

Mbunifu huyo alieza kuwa mwaka huo alipata taarifa kuwa Serikali inafanya shindano la kumtafuta mtu anayeweza kubuni jina moja litakalowakilisha majina ya nchi mbili zilizoungana za Tanganyika na Zanzibar, ndipo alipoamua kuingia katika mchakato huo huku akimtanguliza zaidi Mungu.

Alisema kuwa alichukua kipande cha karatasi pamoja na kalamu yake na kuanza kufanya ubunifu wake, alitumia majina manne kupata jina hilo moja japo mashindano yaliyoeleza kuwa alipaswa kupata jina linalotokana na majina ya nchi hizo mbili.

“Alianza kwa kuandika jina la Allah (Mungu), kisha akaandika jina la Tanganyika, jina la Zanzibar, jina lake pamoja na jina la Kundi la dini yake aliyokuwa akisali wakati huo,” Mtangazaji wa Times FM, Stanslaus Lambart aliyezungumza naye kutoka Uingereza anasimulia.

Mchakato wa kuchanganya majina hayo ulianza kwa kuchukua herufi za mwanzo za Tanganyika, herufi mbili za Zanzibar, herufi moja kutoka kwenye jina lake na herufi nyingine kutoka kwenye jina la kundi la dini yake. Baada ya kusoma jina lililotokea likasomeka ‘Tanzania’.

Anasema aliona jina hilo linatamkika vizuri, na pia akagundua kuwa limechukua ‘Tanzan’ zinazoonesha muunganiko wa Tanganyika na Zanzibar, lakini pia nchi nyingi za Afrika zilikuwa zina majina yanayoishia ‘ia’ mfano Nigeria, Algeria n.k, akaona inafaa zaidi kuwa hivyo.

Iqbal ameeleza kuwa baada ya muda, baba yake mzazi, mzee Mohammed alipokea barua nzito kutoka Serikalini, huenda ilikuwa barua ya kwanza kuipata moja kwa moja kutoka Wizarani ikiwa na jina la mwanae ‘Iqbal’.

Barua hiyo iliyokuwa imesainiwa na Waziri wa Habari ilimueleza kuwa amechaguliwa kuwa mmoja kati ya washindi wa shindano hilo akiwa kati ya washindi 16 waliopatikana na kwamba angelipwa kiasi cha shilingi 12 kati ya keki ya shilingi 200 iliyokuwa imetengwa kwa ajili ya washindi wa shindano hilo.

Hata hivyo, yeye ndiye aliyebaki kuwa mshindi pekee baada ya washindi wengine 15 kutojitokeza, huku kijana mmoja akijitokeza kudai kuwa alikuwa mmoja kati ya washindi, lakini alikosa kigezo muhimu cha kutokuwa na ushahidi wa barua aliyotumiwa.

Serikali iliamua kumpa kiasi chote cha shilingi 200, Mohammed Iqbal kama mshindi pekee aliyejitokeza na jina alilolibuni ‘Tanzania’ likaanza kutumika hadi leo. Ikabadili matumizi ya muungano kuitwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ na kuwa ‘Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’.

Hata hivyo, Mzee Iqbar ambaye hivi sasa anaishi nchini Uingereza lakini hutembelea mara kwa mara Tanzania aliyobuni jina lake, amelalamika kuwa anashangaa hayuko katika orodha za wanaokumbukwa na kutajwa katika historia ya Tanzania kama anavyostahili. Pia, anaona Serikali haimthamini na kuenzi mchango wake wa ubunifu kwa kutomuweka kwenye orodha ya kumbukumbu zinazopewa nafasi ya kutajwa na vizazi vya Tanzania.

Ajabu: Wafanya Mapenzi kwenye kituo cha treni mbele ya abiria (picha)
Zitto: Rais Magufuli ameyapapasa tu majipu haya