Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi, Selemani Jafo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro kumsimamisha kazi Daniel Elimringi Maleki ambaye video yake imesambaa katika mitandao ya kijamii ikimuonyesha akichana na kukanyaga kanyaga kitabu kitakatifu cha dini ya kiislamu ‘Quran’.

Na kumuagiza Mkurugenzi na kamati ya maadili na nidhamu kufanya uchunguzi ili iweze kuchukua hatua stahiki kufuatia kitendo hicho kilichotafsiriwa kuwa ameidharau dini na maandiko yake.

Jafo ametoa agizo hilo jana Ijumaa Februari 7, 2020 mjini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu video hiyo iliyozua gumzo mitandaoni.

Amesema Elimringi ni ofisa biashara wa wilaya hiyo, “mtumishi huyo yupo chini ya ofisi ya Rais Tamisemi, tukio lile ukiliangalia kwenye mitandao ya kijamii halileti afya njema kwa nchi yetu ambayo ina utulivu na amani lakini wananchi wake wanaheshimiana kwa misingi ya imani mbalimbali.”

“Mimi ni waziri ninayesimamia tawala za mikoa na Serikali za mitaa ambayo Halmashauri ya Kilosa ni miongoni mwa halmashauri ninazozisimamia maana yake na mtumishi huyo ni miongoni mwa watumishi walio chini ya Tamisemi. Nimemuagiza mkurugenzi kumsimamisha kazi.”

Aidha, Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro ACP Willboard Mutafungwa amesema kuwa tayari wanamshikilia kijana huyo na tayari amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilosa nakusomewa mashtaka ya kuudhi na kukashifu dini.

Tamko la BAKWATA kwa aliyetemea mate Quran, "Tutulie"
Video: Aliyechana Quran asimamishwa kazi, Membe atamba kuipa darasa kamati ya maadili CCM