Mahakama Kuu nchini Kenya imeiagiza hospitali ya Nairobi kumlipa Ksh 44.5 milioni (zaidi ya Sh 1.1 bilioni za Tanzania), mtu mmoja aliyefanyiwa vibaya upasuaji wa kichwa miaka minne iliyopita.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji George Odunga amesema kuwa mbali na kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya mgonjwa huyo ambaye alikuwa akisumbuliwa na tatizo la maumivu ya kichwa, wazazi wake wanapaswa kupewa Ksh.1 milioni (Sh. 22.9 milioni za Tanzania).

Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama kuhusu kesi hiyo, Daktari Mandu okutuyi aliyongoza zoezi hilo pamoja na Hospitali ya Nairobi watabeba gharama hizo.

Wazazi wa mgonjwa huyo walifungua kesi mahakamani dhidi ya Hospitali hiyo, kufuatia opasuaji aliofanyiwa akiwa kidato cha nne, ambao badala ya kumtibu ulimsababishia tatizo zaidi la ubongo na kwamba hivi sasa tabia zake ni sawa na za mtoto wa umri wa miaka sita.

Ushahidi uliowasilishwa awali mahakamani hapo, ulionesha kuwa mashine zilizotumika katika kufanya zoezi hilo la upasuaji hazikuwa katika hali nzuri, kwa mujibu wa Citizen ya Kenya.

Majina ya mgonjwa na wazazi yamehifadhiwa kwa sababu maalum.

Serikali Mtandao yaainisha changamoto inazokabiliana nazo
Guardiola ainyooshea mikono Liverpool, ‘ni ngumu’