Siku moja baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi , Profesa Joyce Ndalichako kutangaza kuivunja Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU), aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume hiyo, Profesa Tunus Mgaya ameunga mkono uamuzi huo.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kukabidhi ofisi, Profesa Mgaya amesema kuwa anaunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanapata elimu bora.

Profesa Mgaya alikanusha taarifa zilizoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuwa amepinga utumbuaji huo kwa madai kuwa haukufuata sheria na taratibu.

“Mimi nikiwa miongoni mwa watendaji waliopumzishwa kazi, napenda kueleza kuwa sihusiki na taarifa hizo, suala hili limeshapita na kutolewa uamuzi na serikali na tuiache Tume iendelee kufanya kazi,” alisema Profesa Mgaya.

Alimtaka Profesa Ndalichako kuendelea na juhudi anazozionesha katika kuinua ubora wa elimu nchini ili taifa liwe na watu walioelimika vizuri kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kudai Bunge ‘Live’ kwawaponza Zitto, Lissu, Lema, Mdee, Bulaya na Heche, watumbuliwa
Hans Poppe: Hakuna Mchezaji Wa Kigeni Aliyeachwa Simba