Aliyekuwa Rais wa Afghanistan, Ashraf Ghani ambaye sasa yuko mafichoni katika Falme za Kiarabu, ameeleza kuwa alikimbia nchi hiyo ili kuepusha umwagaji damu, huku akikana ripoti kuwa alikimbia na furushi la fedha kutoka Ikulu.

Ghani amekutana na ukosoaji mkubwa wa wananchi na waliokuwa mawaziri wake kwa kukimbia nchi hiyo muda mfupi baada ya wapiganaji wa Taliban kuingia jijini Kabul, Jumapili.

Balozi wa Afghanistan nchini Tajikistan, amemtuhumu Ghani kuwa aliiba kiasi cha $169 milioni zilizokuwa kwenye mfuko wa nchi na kuwataka polisi wa kimataifa kumkamata popote alipo.

“Niliondoka haraka Kabul ili kuhakikisha haigeuki kuwa Yemen au Syria kwa kupigania madaraka, kwahiyo nililazimika kuondoka,” Ghani ameeleza kwenye kipande cha video.

“Niliondoka na nguo chache tu. Hizo juhudi zinazoendelea za kujichafua kwa madai kwamba nilichukua mamilioni ya fedha hazina ukweli wowote. Mnaweza kuwauliza maafisa wa uhamiaji wa uwanja wa ndege,” alisisitiza.

Aidha, Ghani alieleza kuwa anaunga mkono mazungumzo kati ya Taliban na viongozi wa Serikali yake, akieleza kuwa naye yuko katika mazungumzo ya jinsi anavyoweza kurejea Afghanistan.

Sabaya amkana msaidizi wake, atiririka ‘siri’ akijibu maswali
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 19, 2021