Rais wa zamani wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva anakabiliwa na kifungo cha miaka 12 jela kwa makosa ya kupokea rushwa.

Mahakama ya juu nchini humo imemkuta Lula na hatia dhidi ya makosa yanayomkabili na  imeamuru aanze kutumikia kifungo chake licha ya maombi aliyowasilisha akitaka awe huru hadi rufaa yake itakaposikilizwa.

Mwanasiasa huyo amekumbwa na hukumu hiyo wakati ambapo amekwisha tangaza nia ya kuwania urais katika uchaguzi wa mwezi Oktoba mwaka huu huku tafiti nyingi zikionesha kuwa anaongoza dhidi ya wagombea wengine waliotangaza nia.

Akizungumzia hatua hiyo na mwenendo wa kesi yake, Lula amedai kuwa yote yalifanyika kwa lengo la kumkwamisha asigombee tena urais na kwamba yalitungwa makusudi na vyombo vya usalama kwa kushirikiana na Serikali.

Uamuzi wa Mahakama ulitolewa na jopo la majaji 11 ambapo kati yao, majaji sita walimtia hatiani baada ya mwenendo wa muda mrefu wa kesi hiyo iliyovuta hisia za watu wengi.

Wafuasi wake wameendelea kufanya matamasha makubwa kwa lengo la kuhamasisha zaidi watu kupinga mwenendo wa mashtaka dhidi ya mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 72.

Aidha, zaidi ya watu 20,000 waliandamana Jumanne wiki hii katika eneo la Sao Paulo wakitaka Lula afungwe jela haraka. Wakati huohuo wafuasi wake kwa maelfu walifanya pia maandamano kutaka aachiwe huru.

Lula alikuwa rais wa Brazili kati ya mwaka 2003 na 2011.

Walioathiriwa na sakata la Facebook wafika milioni 87
Magazeti ya Tanzania leo Aprili 5, 2018