Mahakama nchini Kenya imemhukumu kifungo cha miezi sita jela mwanaume mwenye umri wa miaka 22 kwa kumtishia, kumkimbiza na fimbo bibi yake mwenye umri wa miaka 60.

Kijana huyo aliyetajwa kwa jina la Lenny Mugendi, amepewa nafasi nyingine ya kulipia faini ya Shilingi za Kenya 20,000 ili akwepe adhabu ya kuishi jela kwa kipindi hicho.

Imeelezwa kuwa Mugendi alifika nyumbani kwao alipokuwa anaishi na bibi yake Lenny Mugendi, Disemba 21 mwaka huu majira ya saa moja usiku. Baada ya kufanya upekuzi wa muda alianza kumuuliza bibi yake kuhusu kilipo kitambulisho chake lakini hakupata majibu.

Mahakama hiyo imeelezwa kuwa alipoona bibi huyo hamjali na anaendelea na shughuli zake, alimtishia kumchapa kwa bakora, ndipo bibi huyo alilazimika kukimbia huku akipiga kelele za kuomba msaada. Hata hivyo, Mugendi hakumuacha aliendelea kumkimbiza hadi alipofika kwenye nyumba ya mama yake mkubwa (mtoto wa bibi huyo).

Mahakama hiyo ilielezwa kuwa baada ya kuondoka, bibi na mwanaye walitoa taarifa polisi na baadaye kijana huyo alikamatwa.

Katika utetezi wake, mshtakiwa huyo aliiambia Mahama kuwa alighafirika baada ya kutafuta kitambulisho sehemu zote ndani ya nyumba hiyo, na alipomuuliza bibi yake hakuonesha kujali.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Jean Ndengeri alisema kuwa mshtakiwa hakuonesha kujutia kufanya kosa hilo ambalo ni tishio la kudhuru mwili na kuvunja amani.

Makala: Ukweli wa chanzo cha Krismas, Upagani na Kuzaliwa Yesu
Jeshi latekeleza hukumu kwa kumuua kwa risasi gaidi wa Al-Shabaab

Comments

comments