Bingwa wa dunia wa mapigano ya  UFC, Khabib Nurmagomedov ambaye alimpiga Conor McGregor hivi karibuni ametangaza ubabe dhidi ya bingwa wa zamani wa masumbwi, Floyd Mayweather.

Khabib ameunguruma mbele ya Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mayweather Promotion inayomilikiwa na bondia huyo tajiri zaidi kwenye mchezo huo, akidai kuwa yeye amefanikiwa kumpiga kirahisi zaidi McGregor tofauti na ilivyokuwa kwa Mayweather.

“Kuna mfalme mmoja tu nyikani. Mfalme mmoja tu ambaye ni mimi hapa. Twende sasa Mayweather, tunatakiwa kupigana,” Khabib alitamba kwenye kipande cha video ambacho kiliwekwa Instagram.

“Mimi ndiye mfalme kwa sababu Mayweather alishindwa kumuangusha McGregor lakini mimi nimemuangusha kirahisi,” aliongeza.

Khabib ambaye ni raia wa Urusi alifanikiwa kumpiga McGregor Oktoba 6 mwaka huu na kuendeleza rekodi ya kutoshindwa pambano lake hata moja kati ya mapambano 27 (27-0).

Mayweather aliwahi kumpiga McGregor akimzimisha katika raundi ya 10 katika pambano lao la Agosti mwaka 2017. Mayweather ana rekodi ya kutoshindwa katika mapambano yake yote 50.

Wiki iliyopita, Khabib alimtembelea Rais wa Urusi, Vladimir Putin aliyemualika Ikulu ili ampongeze kwa ushindi wake dhidi ya McGregor.

Mayweather ametangaza kurejea tena ulingoni kupambana na Manny Pacquiao katika pambano lao la marudiano mapema mwakani. Ataanza kupambana Disemba mwaka huu jijini Tokyo nchini Japan katika mapambano yake ya kufungua njia ya kurejea rasmi ulingoni.

Prince Harry, Meghan waanza ziara ya kikazi Australia
Video: Dau la bilioni 1 latangazwa kupatikana kwa Mo Dewji