Muuguzi mmoja wa hospitali ya Mkoa wa Mbeya anayedaiwa kumkashifu Rais John Magufuli alipokuwa akimhudumia mama wa mgonjwa katika dirisha la dawa amebainika.

Muuguzi huyo ambaye hakutajwa jina na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Gloria Mbwille, amedaiwa kuwa alimtolea maneno ya kashfa, Junes Elias ambaye ni mama wa mgonjwa aliyekuwa hospitalini hapo akitumia jina la Rais John Magufuli.

Juzi, Mama huyo alimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla kuwa Novemba 22 mwaka huu alimpeleka hospitalini hapo mtoto wake aliyemtaja kwa jina la Joyce Asifiwe mwenye umri wa miaka 9, lakini baada ya kukamilisha taratibu zote na kufika katika dirisha la dawa kuchukua dawa hizo aliambulia kashfa.

“Kwenye dirisha hilo nilimkuta muuguzi mmoja ambaye aliniambia kwamba ‘dawa zote zinauzwa. Hapa hakuna dawa za bure, si mlichagua Magufuli, sasa mtaisoma namba’,” mama huyo alimueleza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Kutokana na maelezo hayo, Mkuu wa Mkoa alimuita Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk Ismail Macha kwakuwa Mganga Mkuu hakuwepo, na alimtaka waongozane hadi hospitalini hapo ambapo wauguzi waliokuwa dirisha la dawa siku hiyo ya tukio waliitwa na mama yule alimtambua mhudumu aliyemtolea maneno hayo.

Jana, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Mbwille alisema kuwa tayari imeundwa tume ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili muuguzi huyo kwa ajili ya kuchukua uamuzi sahihi.

Tanzia: Mwanamapinduzi Fidel Castro afariki Dunia
Video: Majaliwa ampa wiki moja Mwakyembe, ni kuhusu mkataba wa Mawakili Afrika Mashariki