Mkuu wa Jeshi la Sudan, Awad Mohamed Ahmed Ibn Auf aliyeongoza kumpindua Al-Bashir na kutangaza utawala wa kijeshi kwa muda amejiuzulu saa chache zilizopita.

Awad ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo ikiwa ni saa 48 tu tangu jeshi la Sudan litangaze kumkamata Bashir na kwamba lingeongoza nchi hiyo kwa kipindi kisichozidi miaka miwili kupisha utawala wa kiraia. Ripoti zimeeleza kuwa jiji la Khartoum limeripuka kwa shangwe kufuatia tangazo hilo.

Februari mwaka huu, Awad alitangazwa kuwa Waziri wa Ulinzi katika baraza jipya la Bashir, na baada ya kumuondoa madarakani alitangaza kuongoza baraza la kijeshi.

Awad amemtangaza Lieutenant General, Abdel-Fatah al-Burhan Abdel-Rahman kuchukua nafasi yake na kuliongoza Baraza la Kijeshi.

Wakati huo, Shirika la Habari la Uturuki, Anadolu, limeripoti kuwa Baraza la Kijeshi la Sudan linatafuta msaada kutoka balozi za kiarabu kutokana na mashinikizo kutoka mataifa ya nje.

Bashiri hivi sasa anashikiliwa na jeshi hilo, lakini jeshi hilo limesisitiza kuwa atafunguliwa mashtaka ndani ya nchi hiyo na kwamba hatapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), nchini The Hague.

Bashir aliyeiongoza Sudan kwa miaka 30, alikuwa anakabiliwa na mashtaka ICC, lakini hadi sasa hakuna nchi yoyote ya Afrika aliyoitembelea iliyowahi kukubali kumkamata.

Utawala wake umefikia kikomo kutokana na maandamano makubwa yaliyozuka yakipinga utawala wake pamoja na ugumu wa maisha. Bashir alikuwa akikabiliwa na vikwazo vingi kutoka mataifa ya Ulaya na Magharibi, hali iliyozidi kuzorotesha uchumi wa taifa hilo.

Taharuki: Kahaba adai hupeleka kwa mganga kondomu alizotumia, wateja wake wafa
AFCON: Tanzania ilivyopangiwa Senegal, Kenya na Algeria