Mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji wa kihistoria wa kupandikizwa figo ameruhusiwa kutoka hospitalini akiwa na afya njema.

Bibi Prisca Mwingira ambaye  alifanyiwa upasuaji mkubwa na wa kwanza kufanyika  hapa nchini alipandikizwa figo Novemba 21, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) chini ya timu ya wataalam wa MNH kwa kushirikiana na watalaam wa Hospitali ya BLK ya nchini India.

Akizungumza na waandishi wa habari leo baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini Bibi Prisca aliwashukuru watalaamu wote walioshiriki katika kumuhudumia  na pia ametumia fursa huyo kumuomba Rais John Magufulu kuendelea kuisaidia MNH ili kuhakikisha huduma za kibingwa wa juu zinaendelea kutolewa katika hospitali hiyo.

“Kipekee namshukuru mwenyezi Mungu, madaktari , wauguzi, uongozi wa Hospitali ya Muhimbili  pamoja na serikali kwa kufanikisha matibabu yangu, nilisumbuliwa na ugonjwa wa figo takribani mwaka mzima na kuingia katika matibabu ya kuchuja damu, lakini hatimaye leo kaka yangu amejitolea figo yake moja na nimewekewa mimi kwa kweli namshukuru sana’’ amesema Mwingira.

Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya figo, Dkt. Jackline Shoo wa Muhimbili alisema upasuaji wa kupandikiza figo ulitumia takribani saa nne na zoezi hilo limekamilika vizuri na mgonjwa anarejea nyumbani  huku afya yake ikiwa salama.

“Mgonjwa anaondoka Hospitalini akiwa mzima salama kabisa , anaenda kujumuika na familia yake ataishi kama binadamu wengine ingawa kuna masharti atatakiwa kuyafuata  kama alivyoshauriwa na wataalam,” amesema Dkt. Shoo.

Pia, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Aminiel Aligaesha amesema upasuaji huo umegharimu Shilingi Milioni 21 na endapo mgonjwa angepelekwa nchini India matibabu yake yangegharimu Shilingi Milioni 80 hadi Shilingi milioni 100.

Serikali kuangalia upya mfumo wa Elimu ya juu
Polepole asema CCM sio daladala, amtaka Wema afuate utaratibu

Comments

comments