Serikali ya Mkoa wa Mara imeitaka muwekezaji aliyeishikilia Musoma Hotel kwa miaka 10 bila kuiendeleza ajisalimishe kwenye ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), licha ya kurudisha Serikalini nyaraka zote za umiliki wa hotel hiyo.

Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima amemtaka mwekezaji huyo, Mahuza Nyakirang’anyi kuhakikisha anajisalimisha Takukuru kabla ya saa nane mchana, ili ahojiwe kwa kuvunja sheria na taratibu za uwekezaji.

Pamoja na Nyakirang’anyi, Mkuu huyo wa mkoa alimtaja pia Otieno Igogo ambaye anadaiwa kumiliki hekari 10 za ardhi ya uwekezaji wa maziwa katika eneo la Utegi wilayani Rorya na baadaye kulitelekeza. Wawili hao watahojiwa leo.

Malima alisema kuwa kama ilivyo kwa Nyakilang’anyi, igogo pia aliwasilisha Serikalini nyaraka zote za umiliki wa eneo hilo lakini bado ana mambo ya kujibu na kuchunguzwa.

“Tuliwapa hoteli wameturudishia gofu, tumewapa shamba zuri wameturudisha uharibifu. Kwahiyo nyaraka walizoleta ni kitu kimoja na kuturidishia mali yetu ni kitu kingine,” Mkuu wa Mkoa Malima anakaririwa na The Guardian.

Nyakirang’anyi na Igogo walitajwa na Rais John Magufuli katika ziara yake ya hivi karibuni katika maeneo ya kanda ya ziwa, ambapo aliwataka kuhakikisha wanarejesha haraka maeneo hayo ya uwekezaji.

Rais Magufuli alisema kuwa wawekezaji hao wazawa wameviweka vyombo vya ulinzi na usalama vya mkoa wa Mara mifukoni mwao ndio sababu wanaweza kufanya hayo.

CUF wakoleza wino wa Chadema kumtaka Maalim Seif Urais 2020
Waitara aondoka 'redioni' baada ya kumuona mgombea wa Chadema