Mwanasheria nguli, Miguna Miguna ambaye alisimamia zoezi la Kiongozi wa NASA, Raila Odinga kujiapisha kama ‘Rais wa Wananchi’ Januari 31, amesema kitendo cha mwanasiasa huyo kutangaza maridhiano na Rais Uhuru Kenyatta ni usaliti kwa wafuasi wake.

Miguna ambaye uamuzi wake wa kusimamia tukio hilo la kuapishwa Odinga pamoja na kujitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) la NASA ambalo Serikali ililitaja kuwa kundi la kihalifu, alisafirishwa kwa nguvu kutoka nchini Kenya kwenda Canada.

“Maridhiano kati ya Uhuru Kenyatta na Raila ni usaliti mkubwa dhidi ya mamia ya wakenya wasio na hatia waliopoteza maisha wakipigania demokrasia na kulinda kura za Raila Odinga zilizoibiwa katika uchaguzi wa mwaka 2007, 2013 na 2017,” imeeleza taarifa ya Miguna kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Amesema kuwa amesikitishwa na uamuzi wa Raila kwakuwa yeye yuko Canada kutokana na kufukuzwa nchini baada ya kusimamia uapishwaji wa Rais katika eneo la Uhuru Park.

“Maridhiano ya kweli ya Wakenya sio kwa watu wawili kushikana mikono bali ni kujenga jamii yenye usawa na haki inayoongozwa kwa sheria, heshima kwa haki za binadamu na kutokomeza rushwa na ukabila,” aliongeza.

Miguna alisisitiza kuwa atarejea nchini hivi karibuni kwa lengo la kuendeleza mapambano kupata haki ya demokrasia ya kweli.

Japan yalalama uamuzi wa Trump juu ya ushuru
Tanzania yaibuka kidedea huduma za fedha jumuishi