Said Mrisho aliyetobolewa macho na kuchomwa visu na mtuhumiwa anayedai kumtambua kwa jina la Salum Njwete maarufu kama Scorpion jana alitoa ushahidi wake kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Mrisho aliieleza Mahakama hiyo kuwa anamtambua mshitakiwa kwakuwa alimuona kabla hajamtoboa macho kwa visu.

Alidai kuwa Septemba 6 mwaka huu, alikuwa anaeleka nyumbani kwake eneo la Makuburi jijini Dar es Salaam, ambapo alitumia usafiri wa bajaji aliyemfikisha eneo la Buguruni kwa mnyamani kwani hakuweza kuendelea na safari.

Alisema baada ya kufika katika eneo hilo, aliwaona wauza kuku ndipo alipoamua kununua kuku mmoja kwa shilingi 6,000 huku mfukoni akiwa na pesa zilizotuna na mkononi akiwa na cheni ya madini ya fedha (silver).

Mrisho aliiambia mahakama hiyo kuwa wakati anaendelea kufanya manunuzi, alimuona mtu aliyekuwa upande wa pili ambaye alimueleza kuwa ana shida, hivyo anaomba amsaidie. Anasema alimtaka mtu huyo kumueleza shida yake pale alipokuwa lakini mtu huyo alikaa kimya.

‘Ghafla nilishtukia ninachomwa visu mkononi na bega la kushoto ambapo nilipogeuka niliendelea kuchomwa na nikaanza kupiga kelele ya mwizi lakini sikupata msaada, kwani nilishangazwa kuona watu wananiona lakini hawanipi msaada,’’alisimulia.

“Yule mtu alijibu ‘hakuna mtu wa kumsaidia’, na aliendelea kumchoma visu vinne tumboni na kuanguka chini. Wakati huo kuna watu walikuwa wanamwita Scorpion, kwamba tayari umeshaua huku akiendelea kunikagua mfukoni,’’aliongeza.

Salum Njwete (Scorpion)

Salum Njwete (Scorpion)

Alisema baadae alimvua fulana na kumfunga kisha kumburuza hadi barabarani akitaka magari yamgonge. Wakati huo Mrisho anadai alikuwa akimuona mtu huyo usoni kwani alikuwa hajamchoma kisu machoni. Kwa mujibu wake, alikaa barabarani bila kugongwa na magari kwa zaidi ya nusu saa, ndipo mtu huyo alipomfuata tena na kumchoma kisu machoni.

Mrisho ambaye ni shahidi namba moja katika kesi hiyo alisema alipata msaada baadae kutoka kwa ‘Wasamalia Wema’ kabla ya kufuata taratibu za kupata PF3 ya Polisi na kufikishwa katika hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu.

Katika maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali, Mshtakiwa anadaiwa kufanya tukio la unyang’anyi wa kutumia silaha Septemba 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Pamoja na kumjeruhi kwa visu mlalamikaji, mshtakiwa huyo ambaye ni mwalimu wa Karate alidaiwa kuiba cheni ya dhahabu gramu 38 yenye thamani Shilingi 60,000, kibangili cha mkononi na fedha kiasi cha shilingi 331,000 pamoja na pochi, vyote vina thamani ya Sh 476,000, mali ya Said Mrisho.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 28 mwaka huu itakaposikilizwa tena mahakamani hapo.

 

 

 

 

 

Mwandishi wa Dar24 akamatwa kwa habari ya ‘DC wa Ludewa kukanusha uzushi’
Zola Arithishwa Mikoba Ya Gary Rowett Birmingham City