Mshambuliaji wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Allan Wanga, amesema kuwa anaweza kuifunga Bidvest Wits ya Afrika Kusini, endapo atapewa nafasi ya kucheza kwenye mchezo huo wa kesho Jumamosi.

Azam FC tayari ipo jijini Johannesburg Afrika Kusini tokea juzi mchana kupambana na timu hiyo katika mchezo wa raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika kwenye Uwanja wa Bidvest kuanzia saa 1.00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu hii wa www.azamfc.co.tz Wanga alisema anajipa matumaini hayo kutokana na kuijua vema Bidvest Wits baada ya kufanya majaribio ya wiki mbili Juni mwaka jana kabla ya kutua Azam FC.

“Nilikuwa mwezi wa sita mwaka jana hapa Bidvest Wits nikafanya nao mazuri kwa wiki mbili kwa sababu walikuwa wametaka kunisaini nikiwa El Merreikh tangu miaka miwili iliyopita baada ya maoezi ikawa wamekubaliana na wakala wangu ili kunisajili lakini wakati huo mama yangu (marehemu) alikuwa amezidiwa na ugonjwa na kibali changu cha kazi hapa kilikuwa hakijatoka.

“Ikabidi nilirudi Kenya nishughulikie kibali hicho ndio ikawa mama yangu (marehemu) amezidiwa kabisa hivyo sikuweza kurudi kwa wakati Afrika Kusini kusaini nao mkataba na ndio dirisha lao la usajili likafungwa wakaendelea mimi nikaja kusaini Azam FC,” alisema Wanga.

Akizungumzia alivyojipanga kwa mchezo huo, Wanga alisema yupo fiti kiakili na yupo tayari kwa mapambano dhidi ya timu hiyo inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL).

“Mchezaji yoyote akicheza na ile timu aliyokuwa nayo kitambo au alifanya nayo mazoezi tuseme, huwaga anajitahidi kabisa kufanya vizuri, iwapo nitapata nafasi ya kucheza nina imani nitafanya vema panapo majaliwa pia nitajitahidi niweze kuwafunga,” alisema.

Nyota huyo wa kimataifa kutoka Kenya, alizungumzia aina ya soka wanalocheza Bidvest Wits na kudai kuwa timu hiyo haichezi soka la pasi kama zilivyo timu nyingine hapa Afrika Kusini bali hucheza zaidi mipira mirefu.

“Bidvest wakianza mpira wanapiga mbele kule kwa washambuliaji halafu wanavamia kutaka kufunga na wakifunga bao moja ni hivyo utakuta wanashinda 1-0, 2-1, hata wakati nilipokuwa hapa tuliweza kucheza mechi ya kirafiki na Ajax ya hapa tukawafuanga mabao 2-1, mimi nikifunga bao moja, hivyo utakuta mara nyingi wanafunga mabao machache kwa sababu mpira wao si ule wa kutengeneza wa kupanga wakati wakishambulia kwani wanacheza mipira mirefu,” alisema.

Wanga aliongeza kuwa: “Nadhani sisi tumejitahidi vizuri na tunatarajia tutafanya vema tukiweza kupata ushindi hapa itakuwa vizuri sana na tukipata bao la ugenini itatusaidia sana watakapokuja kucheza Dar es Salaam, kwa sababu wao wamezoea kucheza jioni kutokana na hali yao ya baridi na kule kwetu kuna joto na jua, hivyo tukipata goli la ugenini itaturahishia kuwafunga kirahisi.”

Mchezo huo wa marudiano utakaopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, utafanyika Machi 20 mwaka huu kuanzia saa 9.00 Alasiri.

Programu ya Azam FC leo jijini hapa itafanya mazoezi muda utakaochezwa mchezo huo kwenye Uwanja wa Bidvest Wits kwa ajili ya kuuzoea uwanja watakaochezea kesho kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linalosimamia michuano hiyo.

Chanzo: Azam FC

Magufuli awaruhusu mawaziri hawa wawili kufanya ziara nje ya nchi
Hans van der Pluijm: Tunahitaji Kushinda Dhidi Ya APR