Mfanyakazi mmoja nchini Australia amefungua mashtaka kwenye mahakama ya rufaa ya nchi hiyo akidai bosi wake alikuwa akimbughudhi ofisini kwa kujamba sana.

Awali, mahakama moja ya chini ilifikia uamuzi kuwa hakukuwa na bughudha yeyote katika suala hilo, lakini David Hingst ambaye ni mlalamikaji anadai kuwa bosi wake wa zamani, Greg Short alikuwa akinyanyuka na kumjambia karibu mara sita kwa siku.

Aidha, Hingst mwenye umri wa miaka 56 ambaye alikuwa afisa utawala katika mji wa Melbourne, aliiishtaki kampuni ya Construction Engineering mwaka 2017, kwa madai kuwa mashuzi hayo yamemsababishia msongo wa mawazo, lakini kesi hiyo ilitupwa Aprili 2018.

Pamoja na kutupiliwa mbali kwa kesi aliyoifungua, Hingst amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo na Jumatatu, Novemba 25 alisikilizwa na Mahakama ya Rufaa nchini humo.

”Nilikuwa nikikaa kwenye chumba kidogo ambacho hakina madirisha, alikuwa akiingia bosi wangu na kujamba nyuma yangu na kisha kwenda zake, alikuwa akifanya hivyo mara tano mpaka sita kwa siku,”amesema Hingst alipokuwa akizungumza Shirika la Habari la nchi hiyo, Australian Associated Press (APP).

Kwa upande wake mlalamikiwa katika kesi hiyo, Greg Short ambaye alikuwa bosi wa Hingst amesema kuwa hakumbuki kujamba akiwa karibu na Hingst lakini amesema inawezekana ilitokea mara moja au mara mbili.

Kwa mujibu wa mitandao ya Australia, Hingst amedai kuwa, tabia ya Short ilikuwa ni sehemu ya mpango wa kumng’oa kazini na muda aliofanya kazi na Construction Engineering kulimsababishia msongo wa mawazo, pia amedai kuwa Short alikuwa akimkejeli kutokana na ufanisi wake.

Jeshi la Polisi lazuia mkutano wa ACT- Wazalendo
Video: Zitto ajibu hoja tatu za Msajili, CUF wampokonya Maalim Seif ofisi Zanzibar