Jeshi la polisi nchini Kenya, linamsaka mwanaume mmoja mkaazi wa kijiji cha Wina, Elburgon,  Kaunti ya Nakuru kwa kosa la kumuua baba yake mzazi kwa madai ya kushindwa kumlipa deni la Ksh. 100.

Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na familia hiyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 30 aliingia kwenye malumbano na baba yake, mzee Wilson Chepkicho Yegon, akimdai Ksh. 200 alizomkopesha.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa Mzee Yegon mwenye umri wa miaka 66 alimlipa mwanaye  Ksh. 100 na kuahidi kumalizia kiasi kingine hapo baadaye.

Mwanafamilia mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kobilo Chepyegon aliyezungumza na Citizen ya Kenya, alisema kuwa baada ya kutoridhishwa na kiasi alichopewa, alianza kumshambulia baba yake kwa ngumi na mateke, na mwisho alimpiga na shoka hadi kufa.

Kwa mujibu wa majirani, mtuhumiwa huyo alikuwa na tabia ya kuwapiga wazazi wake wote wawili mara kadhaa.

Akithibitisha tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Nakuru, Naftali Korir ameeleza kuwa jeshi hilo limeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo, na kwamba mwili wa marehemu umepelekwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu.

Kaimu Kamanda Korir  amesema msako wa Jeshi hilo utamnasa mtuhumiwa huyo; na amewaasa wananchi kutojichukulia sheria mikononi.

Zitto adai CCM inaweza kufutwa muswada ukipita ulivyo
Tido kurudishwa Mahakamani, Jamhuri wakata rufaa