Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linamsaka mganga wa jadi, Dela Megejuwa Lwaho mwenye umri wa miaka 44, kwa kusababisha kifo cha mtoto wake Juma Dela Megejuwa mwenye umri wa miaka 12 na watu wengine wawili kuzirai baada ya kuwapa dawa ya miti shamba inayodhaniwa kuwa na sumu ili wasafishiwe nyota zao.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo Januari 18,2021 Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, amesema tukio hilo limetokea Januari 16, 2021 majira ya saa tisa na nusu alasiri katika kijiji cha Mwaningi kata ya Bulige wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Amesema kuwa wawili walio zirai walikimbizwa kituo cha afya cha Chela kwa matibabu na hali zao zinaendelea vizuri.

Aidha, amesema mtuhumiwa (mganga wa jadi) alikimbia mara baada ya tukio hilo na mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kahama kwa uchunguzi zaidi.

Kamanda Magiligimba ametoa wito kwa waganga wa jadi kuwa na uhakika na matumizi ya dawa zao pamoja na matumizi mazuri ya vibali/leseni zao ili kuepuka kusababisha vifo na madhara kwa wateja wao na jeshi la polisi halitamwonea  mganga yeyote anayekwenda kinyume na maelekezo ya vibali/leseni zao.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Januari 19, 2021
Mbunge Chadema 'aula' Kamati ya Bunge