Aliyekua nahodha na kiungo shupavu wa mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona Andres Iniesta, ameungana na mshambuliaji wa sasa wa klabu hiyo Luis Suarez kwa kumtaka Ousmane Dembele kubadilika haraka, ili kufanikisha ndoto za kuwa mchezaji mkubwa duniani.

Iniesta ambaye kwa sasa anasukuma soka kwenye klabu ya Vissel Kobe inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Japan (J1 League), amesema kwa muda sasa amekua akifuatilia sakata la mshambuliaji huyo kutoka nchini Ufaransa na amebaini kuna tatizo linalomsumbua hadi kufikia hatua ya kuonekana hana nidhamu.

Amesema hajui ni nini chanzo lakini anaamini ni hali ya kibinaadamu, ambayo inaweza kumtokea mchezaji yoyote, lakini alichokizungumza kuhusu Dembele ni uwezo wake wa kucheza soka, ambao hauendani na matukio anayoyafanya kwa sasa.

Iniesta alibahatika kuzungumzia sakata la kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21 alipohojiwa na kituo cha Radio cha Catalunya mjini Barcelona, ambapo amesema kuna haja ya Ousmane kubadilika na kurejea katika hali yake ya kawaida.

“Dembele ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa kisoka, aliposajiliwa FC Barcelona niliamini klabu imepata mshambuliaji hodari ambaye atakuwa na uwezo mkubwa wa kusukuma mbele gurudumu la mafanikio,” Alisema Iniesta.

Ousmane Dembele

“Nimekua nikifuatilia kuhusu sakata hili, lakini mpaka sasa sifahamu nini kimemsibu Ousmane, kubwa ninalomsihi aachane na mambo anayoyafanya kwa sasa, arudishe mawazo yake katika uwajibikaji ili heshima yake ionekane akiwa na FC Barcelona.”

“Wakati mwingine ni hali ya kibinaadamu inaweza kumbadilisha mtu, lakini ninaamini hakuna jambo linalokosa mwisho, ushauri unaendelea kutolewa dhidi yake, ninaamini atabadilika na kuisaidia FC Barcdelona ambayo bado inamuhitaji kwa kiasi kikubwa.”

Usiku wa kuamkia jana mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Luis Suarez alizungumza na waandishi wa habari jijini Paris na aliulizwa kuhusu Ousmane Dembele, kubwa alilomsihi mchezaji huyo ni kuiga mazuri kutoka kwa wachezaji wenzake wa FC Barcelona, ili kuondokana na kadhia inayomsibu katika kipindi hiki.

Suarez alisema mshambuliaji huyo, kama hatokua tayari kubadilika ataendelea kuwa kwenye wakati mgumu wa kutimiza ndoto zake za kucheza soka la ushindani kwenye kikosi cha kwanza cha Barcelona.

Inadaiwa Dembele amekua anashindwa kubadilika kila anapopewa nafasi, jambo ambalo limemfanya meneja wa Barca Ernesto Valverde, kuwasilisha mapendekezo ya kutaka mshambuliaji huyo auzwe mwezi Januari.

Taarifa zilizotolewa na vyombo hivyo vya habari zinaeleza kuwa, Dembele amekua hafiki kwa wakati mazoezini na amekua na uhusiano hafifu na wachezaji wenzake, jambo ambalo limeanza kuzua taharuki klabuni hapo.

Dembele bado hajaonyesha uwezo wake kisoka tangu alipotua FC Barcelona akitokea Borussia Dortmund mwaka 2017, na haijafahamika nini kinachomsibu hadi kufikia hatua ya kuonyesha utovu wa nidhamu.

Usajili wake uliigharimu FC Barcelona Euro milioni 105 sawa na dola za kimarekani 119.01, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na mshambuliaji kutoka Brazil Neymar, aliyetimkia PSG.

Hakimu ataka kesi ya Mdee imalizike ndani ya mwaka huu
USSF wampigia hesabu Julen Lopetegui

Comments

comments