Aliyekua Meneja wa Mabingwa wa Soka nchini Italia Inter Milan Antonio Conte, ameahidiwa na Uongozi wa Klabu ya Tottenham Shilingi bilioni 471 kama pesa za usajili, endapo atakubali kufanya kazi na klabu hiyo ya jijini London.

Spurs inahusishwa na taarifa za kumuajiri Meneja huyo kutoka nchini Italia, baada ya kuachana na Nunu Espirito Santo jana Jumatatu (Novemba Mosi), kufuatia mambo kumuendea mrama tangu alipoanza kazi mwanzoni mwa msimu huu 2021/22.

Chini ya Meneja huyo kutoka nchini Ureno Spurs imeshinda michezo mitano na kufungwa mitano kati ya michezo kumi ya Ligi Kuu ya England msimu huu, na kujikuta ikiwa nafasi ya 9 na alama zake 15, ikiwa ni tofauti ya alama 10 dhidi ya vinara wa Ligi Chelsea yenye alama 25.

Conte anatajwa kukaribia kusaini mkataba wa miezi 18 (sawa na mwaka mmoja na nusu), ambao utamuwezesha kukinoa kikosi cha Spurs ambacho kinakabiliwa na mtihani wa kusaka ubingwa wa England.

Meneja huyo ambaye aliwahi kuzinoa klabu za Juventus, Chelsea, Inter Milan na timu ya taifa ya Italia anatarajiwa kutangazwa wakati wowote kuanzia leo Jumanne (Novemba 02) kuwa Mkuu wa Benchi la Ufundi la Tottenham, huku akitegemea kufanya mabadiliko ya kikosi itakapofika mwezi januari (Dirisha Dogo).

Katika misimu miwili Antonio Conte akiwa na klabu ya Chelsea kati ya mwaka 2016 hadi 2018 alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England na ubingwa wa kombe la FA.

Conte kwa sasa hana kazi baada ya kuachana na Inter Milan mwishoni mwa msimu uliopita, akishinda ubingwa wa Ligi Kuu nchini Italia.

Chuku: Tunajua mashabiki wanachokitaka
Nani kasema Diamond Platnums ni mtu mbaya?