Matajiri wa jijini London, Chelsea FC wanajipanga kutuma ofa ya kutaka kumsajili beki na nahodha wa klabu ya Real Madrid, Sergio Ramos.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye garida la Don Balon, Chelsea wamejipanga kuwasilisha ofa hiyo ambayo inakadiriwa kufikia kiasi cha Pauni million 63.5, ambacho kitakua na thamani zaidi kuliko usajili wa mchezaji yoyote nchini England.

Taarifa hizo zimeendelea kufafanua kwamba, Chelsea wapo tayari kufanya hivyo kutokana na msisitizo wanaoupata kutoka kwa meneja wao mpya kutoka nchini Italia, Antonio Conte ambaye anataka kukisuka upya kikosi cha The Blues.

Ramos, mwenye umri wa miaka 30, amedumu kwa miaka 11 akiwa na klabu ya Real Madrid na amekua sehemu ya vikosi vya nyakati tofauti vilivyopata mafanikio katika ligi ya nchini Hispania pamoja na barani Ulaya.

Hata hivyo inadhaniwa kwamba huenda Chelsea wakapata wakati mgumu wa kumng’oa beki huyo pale Stantiago Bernabeu, kutokana na jina lake kutokuwepo katika orodha ya wachezaji ambao wamependekezwa kuondoka mwishoni mwa msimu huu.

Meneja wa Real Madrid, Zinedin Zidane, amekua akimuamini sana Ramos katika kikosi chake ambacho kwa siku za hivi karibuni kimeonyesha kufufua matumaini ya kuwania ubingwa wa nchini Hispania mwa msimu wa 2015-16.

Tetesi za kutumwa kwa ofa ya Sergio Ramos, zinaashirikia safari kwa beki na nahodha wa Chelsea, John Terry ambaye mkataba wake utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Tayari kuna taarifa zinaeleza kwamba Terry ataondoka Stamford Bridge mwishoni mshoni mwa msimu huu na kutimkia nchini China, lakini vyombo vingine vya habari vinaeleza kuwa, beki huyo mwenye umri wa miaka 35 ataelekea nchini Marekani kucheza ligi ya MLS.

Luis Enrique: Lawama Zielekezwe Kwangu, Sio Kwa Wachezaji
Pep Guardiola Kuizidi Kete Man utd Kwa Nikola Maksimovic?