Majaaliwa ya mshambuliaji kutoka nchini Brazil, Alexandre Pato ya kuendelea kucheza ndani ya kikosi cha Chelsea, yapo mikononi mwa meneja mpya wa klabu hiyo Antonio Conte.

Wakala wa mshambuliaji huyo aliyesajiliwa huko Stamford Bridge mwezi januari mwaka 2016, Gilmar Veloz amesema mpaka sasa wanasubiri maamuzi ya Conte ambaye yupo na kikosi cha timu ya taifa ya Italia kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Euro 2016.

Veloz, amesema tumaini lake kubwa kwa mshambuliaji huyo lipo mikononi mwa meneja huyo kutoka nchini Italia, kutokana na kuamini bado kuna uwezekano wa Pato kuendelea kubaki klabuni hapo.

Amesema anatambua Antonio Conte atahitaji kuanza na mipango ya kuwatumia wachezaji atakaowasajili na wale watakaobaki kikosini, hivyo anaamini Pato ni miongoni mwa watakaosubiri kauli ya mwisho ya mtaliano huyo.

Hata hivyo tayari baadhi ya wachezaji wa Chelsea wameshahakikishia nafasi ya kuendelea kubaki klabuni hapo, huku wengine wakitambua wazi hawana nafasi ya kuendelea kucheza soka ndani ya The Blues.

Mshambuliaji kutoka nchini Hispania, Diego Costa ana matarajio makubwa ya kuendelea kusalia klabuni hapo, licha ya kuhusishwa na taarifa za kuhitajika katika klabu yake ya zamani ya Atletico Madrid, huku mshambuliaji kinda Bertrand Traore akiwa na matumaini kama hayo kufuatia uwezo wa kufunga mabao manne aliouonyesha wakati wa msimu wa 2015-16.

Mshambuliaji kutoka nchini Colombia, aliyekua akicheza kwa mkopo klabuni hapo Radamel Falcao tayari imeshafahamika anaondoka na kurejea katika klabu yake ya AS Monaco ya Ufaransa huku kukiwa na mashaka kwa mshambuliaji Loic Remy.

Pia kumekua na majina ya washambuliaji wanaotajwa huenda wakasajiliwa klabuni hapo kama mshambuliaji wa SSC Napoli, Gonzalo Higuain pamoja na Antoine Griezmann wa Atletico Madrid.

 

Ronald Koeman Kusaini Mkataba Mpya Kwa Masharti
Majaliwa atoa onyo kali, akazia nguvu msako wa wala Rushwa, Mafisadi