Meneja mpya wa klabu ya Chelsea, Antonio Conte amepanga kuanza kumsajili beki wa klabu bingwa nchini Italia, Leonardo Bonucci, kufuatia pengo ambalo litaachwa na nahodha John Terry mwishoni mwa msimu huu.

Conte ambaye aliidhinishwa kuwa meneja mpya wa The Blues, baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu hapo jana, amepanga kufanya hivyo kutokana na kuamini, Terry hatokua na nafasi ya kuendelea klabuni hapo kutokana na mkataba wake kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Conte, anaamini akifanikiwa kumsajili Bonucci, kutakua na mtazamo tofauti katika safu yake ya ulinzi ambayo itakuwa na shughuli ya kuitetea Chelsea katika kila mchezo watakaocheza msimu ujao wa ligi.

Mpaka sasa Terry, ameshinsdwa kutoa jibu kama atakuwa tayari kuanza mazungumzo ya kusaini mkataba mpya, licha ya kuthibitishiwa kuwa ana nafasi ya kuendelea na meneja wa muda wa Chelsea, Guus Hiddink.

Endapo Conte atahitimisha suala la Bonucci, Chelsea watalazimika kutoa kiasi cha Pauni million 25 kama ada yake ya usajili wa kumuhamisha kutoka Juventus Stadium mpaka Stamford Bridge.

Bonucci aliwahi kufanya kazi na Conte, wakati wa utawala wa meneja huyo ambao ulishuhudia akiisaidia Juventus ikitwaa ubingwa wa nchini Italia (Scudetto) mara tatu mfululizo (2011–12, 2012–13, 2013–14).

Beki huyo mwenye umri wa miaka 28, alijiunga na Juventus mwaka 2010 akitokea kwenye klabu ya Bari kwa ada ya uhamisho wa Euro million 15.5, na tayari ameshaitumikia The Old Lady katika michezo 191 na kufunga mabao 11.

Inter Milan yajizatiti Kwa Yaya Toure
Kamati ya Bunge yaibana TCRA kwa kutumia mabilioni kujilipa posho na safari