Kampuni ya Apple jana iliweka rekodi ya kuwa kampuni ya kwanza duniani kufikisha thamani ya $1 trilioni, baada ya hisa zake kushika hatamu sokoni ikifika kilele cha mauzo cha $207.05 kwa hisa.

Kwa mujibu wa ripoti ya soko la hisa, hisa za Apple zilipanda zaidi tangu Jumanne wiki hii baada ya kuripotiwa kuwa kampuni hiyo imepata mafanikio makubwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu.

Kwa hatua hiyo, Apple imezifunika kampuni ambazo ni washindani wake wakuu, Amazon na Microsoft kwa kuwa kampuni ya kwanza kufikia thamani ya $1 trilioni.

Mafanikio ya Apple yalianza kuonekana kushika kasi tangu mwaka 2007 baada ya kuzindua simu aina aina ya iPhone ambapo ilipata ongezeko la mauzo ya hisa kwa 1,100%, na baadaye kuongezeka mara tatu zaidi mwaka jana.

Kampuni ya Apple iliyoanzishwa na Steve Jobs mwaka 1976 ilianza kufahamika zaidi kwa kutengeneza ‘kompyuta’ aina ya Mac kabla ya kuzindua pia simu hizo za kisasa na za kipekee ambazo ziliiongezea nguvu ya kiuchumi.

Jobs alifariki mwaka 2011 akiwa ameitabiria mafanikio makubwa kampuni hiyo ambayo sasa iko chini ya Mtendaji Mkuu, Tim Cook. Aliipigia mstari iPhone kuwa ni chanzo kikuu cha mafanikio ya haraka ya kampuni hiyo kiuchumi na ndivyo ilivyokuwa.

Mwaka jana, mauzo ya kampuni hiyo yalifikia $229 bilioni, ikiwa na faida ya $48.4 bilioni, hali iliyoifanya kuwa kampuni ya Kimarekani iliyotengeneza faida kubwa zaidi.

Meya Boniface akomaa na ‘aliyemdanganya’ Rais kuhusu mapato
Terry Butcher aitema Azkals (Street Dogs)

Comments

comments