Kikosi cha Argentina kimeanza vibaya harakati za kusaka Taji la Dunia kwa kufungwa 2-1 na Saudi Arabia katika mchezo wa Kwanza wa Kundi C, uliopigwa Uwanja wa Lusail Iconic, mjini Lusail.

Argentina iliyokua ikipewa nafasi kubwa ya kushinda mchezo huo, ilianza kupata bao la kuongoza kwa mkwaju wa Penati uliopigwa na Nahodha na Mshambuliaji wao Lionel Messi dakika ya 10.

Saudi Arabia walifanikiwa kusawazisha dakika ya 48 kupitia kwa Al-Shehri, na dakika tano baadae wakaongeza bao la pili na la ushindi S. Al-Dawsari.

Kwa ushindi wa leo, timu ya taifa ya Saudi Arabia imevunja rekodi ya Argentina ya kutofungwa katika mechi 36 zilizopita za mashindano yote.

Pia Saudi Arabia imekuwa timu ya kwanza nje ya bara la Ulaya kuifunga Argentina kwenye Kombe la Dunia tangu Cameroon ilipofanya hivyo mwaka 1990.

Kwa matokeo hayo Saudi Arabia anakwea kileleni mwa msimamo wa Kundi C, akisubiri matokeo ya mchezo wa pili wa Kundi hilo kati ya Mexico na Poland ambao utapigwa saa moja usiku kwa saa za Afrika Mashariki, katika Uwanja wa 974, mjini Doha.

Polisi yazungumzia zoezi uteketezaji wa silaha
UNRSF yalia na ajali za barabarani kwa watoto