Rais wa shirikisho la soka nchini Croatia (HNS) Davor Suker, amesema amepokea ujumbe wa pongezi kutoka kila kona ya dunia, kufuatia kikosi cha timu ya nchi hiyo kufanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya michuano ya kombe la dunia kwa kufikisha alama tisa, ambazo zinawafanya kuongoza msimamo wa kundi D.

Pongezi kwa kiongozi huyo wa soka nchini Croatia ambaye alikiongoza kikosi cha nchi hiyo kama nahodha wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 1998, zilianza kuminika baada ya mchezo wa mwisho wa kundi D uliochezwa usiku wa jana dhidi ya Iceland ambao walikubali kubugizwa mabao mawili kwa moja.

Suker amesema pongezi nyingi alizozipokea zinatoka kwa wadau wa soka nchini Argentina ambao timu yao ya taifa ilipangwa kundi moja na Croatia, na zilipokutana juma lililopita, Vatreni (The Blazers) walichomoza na ushindi wa mabao matatu kwa sifuri.

“Mpaka sasa ni Uruguay na sisi ndio tumemaliza michezo ya makundi tukiwa na alama 9, tumeonyesha uwezo mkubwa katika fainali za mwaka huu,” alisema gwiji huyo aliyeacha kumbukumbu ya kuitumikia timu ya taifa ya Croatia katika michezo 69 na kufunga mabao 45.

“Nimepokea ujumbe mpufi wa simu kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ukitupongeza kwa mafanikio tuliyofikia hadi sasa huko nchini Urusi, na asilimia kubwa waliotupongeza ni wadau wa soka kutoka Argentina.

Alipoulizwa kama [Diego] Maradona ni sehemu ya waliotoa pongezi hizo Suker alijibu “Usinitajie jina la huyo mtu, hapa ninazungumzia mashabiki wa soka wa Argentina waliotambua uwezo wa soka tulilolionyesha katika fainali za mwaka huu.”

Kufuatia kumaliza kinara wa kundi D, Croatia watapambana na mshindi wa pili wa kundi C ambaye ni Denmark katika mchezo wa hatua ya 16 bora utakaochezwa jumapili, huku Ufaransa wakitarajia kupambana na Argentina katika hatua  hiyo.

Jose Mourinho kuivurugia Liverpool kwa Nabil Fekir
RC Wangabo ashauri gereza kutumia ekari elfu 11 kwa kilimo cha alizeti na kahawa