Mashabiki wamezua gumzo mtandaoni baada ya kuwekwa wazi kuwa Ariana Grande amelipwa mara mbili zaidi ya Beyonce kwa ajili ya kutumbuiza kwenye tamasha a Coachella kama msanii anayeliongoza tamasha hilo (headlining).

Ariana ambaye amepanda kwenye jukwaa hilo mwaka huu akiongoza show ameripotiwa na Variety kuwa alilipwa $8 milioni huku Beyonce ambaye alipanda kwenye jukwaa hilo mwaka jana kuliongoza alilipwa $4 milioni.

Tatizo sio tu tofauti ya kiwango cha fedha zilizotolewa na tofauti ya ukubwa wa wasanii hao wawili kwenye ulimwengu wa muziki, mashabiki wameenda mbali na kulinganisha kazi iliyofanywa na wasanii hao ambao wote waliandika rekodi mpya kwenye jukwaa hilo. Ariana amekuwa msanii mdogo zaidi wa kike kuongoza tamasha hilo katika historia wakati Beyonce mwaka jana aliandika rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa kike mweusi kuliongoza tamasha hilo.

Katika tamasha la mwaka jana, Beyonce alipanda na wachezaji 100 na kufanya kazi ambayo iliwafanya mashabiki kubadili jina la tamasha hilo kutoka Coachella kuwa Bey-Chella. Hali hiyo imewafanya mashabiki kujiuliza maswali mengi imekuwaje mwaka huu Ariana ameweza kumpiku kwa malipo.

Wengine waliopima kazi za wasanii hao wamedai kuwa Beyonce alichora mistari ya moto kwenye jukwaa hilo lakini Ariana ambaye ameimba nyimbo nyingi kutoka kwenye albam zake tano alitumbuiza vizuri lakini hakukuwa na jipya tofauti na matamasha yake ya kawaida. Ariana aliwashika watu na ngoma za ‘Sweetener’ ya mwaka 2018 na zile za ‘Thank U, Next’ ya mwaka 2019.

Wiki hii, Beyonce aliachia makala maalum ya namna alivyoshiriki tamasha la Coachella aliyoiita ‘Homecoming’ ambapo ndani ya makala hiyo alionesha jinsi alivyofanya maandalizi kwa miezi nane kwa ajili ya show hiyo aliyoifanya kwa saa mbili.

“Sitafanya tena kazi kubwa kiasi hiki tena kwenye maisha ya muziki wangu,” Beyonce anazungumza kwenye sehemu ya makala hiyo alipokuwa akizungumzia jinsi alivyofanya maandalizi.

Baadhi ya mashabiki wameenda mbali na kudai kuwa wanadhani huenda suala la ubaguzi wa rangi pia linaweza kuwa limechangia kutoa malipo hayo kwa lengo la kuongeza ukubwa wa Ariana kumzidi Beyonce ambaye ana asili ya Afrika.

Mjadala bado unaendelea na umezua mengi mitandaoni. Wewe pia unaweza kufuatilia na kutoa maoni yako, Ariana na Beyonce kupimwa kwa kiwango hicho cha fedha kwa kazi moja ni sawa? Au biashara ni makubaliano, Ariana alifanya vizuri zaidi kwenye makubaliano?

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Aprili 20, 2019
Nicki Minaj aitosa menejimenti yake