Baada ya kuvuliwa ubingwa wa Kombe La Shirikisho Tanzania bara (ASFC) kwa kufungwa na Simba SC mabao mawili kwa sifuri kwenye mchezo wa Robo Fainali, kocha wa Azam FC Aristica Cioaba, amesema wamedhamiria kuhakikisha wanamaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ili kuweka heshima.

Azam FC kesho Jumatano itacheza dhidi ya Mtibwa Sugar mkoani Morogoro kwenye mchezo wa mzunguuko wa 35 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na tayari kikosi chao kimeshaondoka jijini Dar es salaam kwa mtanange huo.

Akizungumza kabla ya kuanza safari ya kuelekea Morogoro kocha Cioaba alisema anaendelea kuimarisha mikakati ili kikosi chake kifanye vema katika michezo iliyobaki licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wake nyota wa kikosi cha kwanza.

Cioaba alisema baada ya kutolewa katika mashindano ya Kombe la FA, nguvu zao zimeelekea katika kulinda heshima yao katika ligi hiyo ambayo mwakani itashirikisha timu 16 tu.

“Tumepoteza nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa, hali hiyo haitaturudisha nyuma kupambana kutafuta alama tatu katika mechi zetu zote zilizobaki, wachezaji wanalifahamu hilo, tutapambana timu kutafuta matokeo mazuri,” alisema Cioaba.

Aliongeza anafahamu hakuna mchezo rahisi kwa sababu kila timu inahitaji kutimiza malengo yake, huku vita kubwa ikiwa kwenye klabu zinazopambana kujinasua na janga la kushuka daraja.

“Wachezaji wanatakiwa kujituma kwa sababu hatujafikia malengo yetu, vijana wangu walicheza vizuri dhidi ya Mwadui FC, matokeo yake yametuimarisha na tunataka kuendeleza kasi ile,” aliongeza kocha huyo.

Azam FC ina alama 65 na iko katika nafasi ya pili kwenye msimamo nyumba ya mabingwa Simba SC yenye alama 81, Young Africans anashika nafasi ya tatu, huku kila timu ikibakiwa na michezo minne kumaliza msimu 2019/20.

Young Africans kumuadhibu Morrison
Wasiovaa barakoa kupigwa faini Sh.263,000 – Uingereza