Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amerejea jijini Dar es salaam sambamba na Kocha wa Viungo, Costel Birsan, wakitokea mjini Frankfurt, Ujerumani walipopata usafiri wa ndege wa kuja Tanzania.

Wawili hao waliwasili Jana Jumatatu jioni, na leo jioni wataanza rasmi majukumu yao ya kukiweka sawa kikosi cha Azam FC, tayari kwa mshike mshike wa ligi kuu msimu huu wa 2019/20, ambao utaendelea kuanzia Juni 13.

Hata hivyo tayari kikosi cha Azam FC kilikuwa kimeanza mazoezi tangu Jumatano iliyopita chini ya Kocha Msaidizi, Bahati Vivier, ambaye aliwasili nchini akitokea nchini kwao Burundi siku chache kabla ya kuanza kazi.

Katika mazoezi chini ya kocha Bahati, Azam FC walifanyia kazi zaidi mazoezi ya mbinu na ufundi kwa kuchezea mpira zaidi kuliko kufanya mazoezi ya viungo kama ilivyokuwa siku za mwanzoni.

Azam FC walifanya mazoezi hayo huku ikiwakosa wachezaji wake Obrey Chirwa, Donald Ngoma na Razak Abarola ambao wamekwama nchini mwao kutokana na mipaka na safari za kutoka nje ya nchi kufungwa katika nchi hizo.

Kikosi cha Azam FC kitaendelea na ligi kuu msimu huu kwa kucheza mchezo wa Kiporo dhidi ya Mbao FC unaotarajiwa kupigwa tarehe 14 ya mwezi huu katika dimba la Azam Complex, saa 1.00 usiku.

Frank Lampard kuingia vitani
Simba SC waingia hatua mpya