Klabu ya washika mtutu wa Emirates, Arsenal jana walimsaidia kocha wao, Unai Emery kufuta tope la woga dhidi ya wapinzani wao, wakimfunga Leicester 3-1.

Kabla ya ushindi huo, Unai Emery alizungumza na vyombo vya habari na kueleza kuwa anaamini timu yake ina mapungufu hasa yaliyoonekana katika baadhi ya mechi za ufunguzi.

“Tunaanza mechi na labda nguvu kidogo zaidi tulizohitaji. Ni kitu ambacho tunahitaji kukiboresha katika mechi zetu zijazo, tukianza na mchezo wa usiku huu dhidi ya Leicester,” alisema meneja Emery.

Hata hivyo, timu hiyo haikuonesha udhaifu huo uliompa mashaka kocha huyo. Katika mchezo wake huo wa tisa na wa saba kwa ushindi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, timu hiyo ilianza kwa sare katika kipindi cha kwanza na kuondoka na ushindi baada ya kipyenga cha mwisho.

Nahodha wa timu hiyo, Mesut Ozil alionesha kiwango cha hali ya juu kubeba jahazi la timu yake wakiwa nyumbani na kuifanya timu hiyo kung’ara kuanzia dakika ya 40 ya mchezo.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Arsenal mbele ya kisiki cha Leicester chini ya mbinu mpya za Claude Puel ambaye kwa mara ya kwanza alibadili mbinu za kujilinda na kushambulia.

Hali hiyo iliifanya Leicester kupata mtaji wa goli moja baada ya beki wa Arsenal, Héctor Bellerín kujifunga.

Hata hivyo, Ozil alisawazisha katika dakika ya 45 na baadaye Mgaboni Pierre-Emerick Aubameyang kupeleka kilio kwa wapinzani wao akipachika magoli mawili katika dakika ya 63 na 66.

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kuwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ikimiliki alama 21, ikifungana na Chelsea ambayo hata hivyo inaizidi kwa magoli ya kufunga.

Leo ni leo Man Utd Vs Juventus: Sanchez nje, Ronaldo ndani
Mo Dewji arejea rasmi mtandaoni na ujumbe

Comments

comments