Kiungo wa klabu ya Arsenal Francis Coquelin, atakuwa nje ya uwanja kwa majuma manne, kufuatia majeraha ya nyama za paja aliyoyapata usiku wa kuamkia juzi.

Coquelin alishindwa kuendelea na mchezo wa ligi kuu ya soka nchini England dhidi ya Bournemouth ambao ulimalizika kwa sare ya mabao matatu kwa matatu katika uwanja wa Dean Court.

Arsene Wenger amethibitisha taarifa za kiungo huyo, huku akitarajiwa kuwa na ukame wa wachezaji wanaocheza nafasi hiyo kwa kipindi cha mwezi mmoja, kufuatia Mohamed Elneny kujiunga na kikosi cha Misri ambacho kinajiandaa na fainali za Afrika za mwaka 2017 zitakazofanyika nchini Gabon.

Kutokuwepo kwa viungo hao wawili, kunakifanya kikosi cha Arsenal kusaliwa na viungo wawili Granit Xhaka na Aaron Ramsey ambao wanacheza katika kikosi cha kwanza huku Santi Cazorla akiendelea kuwa majeruhi.

Hata hivyo Wenger amesema anajua namna ya kufanya kukabiliana na tatizo hilo, na anaamini atafanikiwa kukamilisha mipango ya kukiwezesha kikosi chake kucheza na kufikia lengo.

Katika hatua nyingine mshambuliani Danny Welbeck anatarajiwa kurejea dimbani mwishoni mwa juma hili katika mchezo wa kombe la FA dhidi ya Preston North End.

Wenger amewaeleza waandishi wa habari kuwa, mshambuliaji huyo yupo tayari kucheza baada ya kukosekena kwa zaidi ya miezi sita iliyopita kufuatia jeraha la goti.

Marco Silva Akubali Kubeba Mzigo
Kinana asema CCM itaendelea kushinda chaguzi zote