Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amekubali kushindwa katika harakati za usajili wa mshambuliaji wa klabu bingwa nchini England Leicester City, Jamie Vardy.

Vardy, jana alitangaza maamuzi ya kuendelea kusalia na klabu hiyo kwa kukubali kusaini mkataba mpya wa miaka minne, hatua ambayo ilidhihirisha mipango ya Arsenal ya kutaka kumsajili kwa Pauni milioni 20, tangu majuma matatu yaliyopita imefikia tamati.

Wenger, amekubali kushindwa katika harakati hizo, alipohojiwa na kituo cha televisheni cha beIN Sports, ambapo alisema: “Ninaamini Leicester wamefanya maamuzi mazuri ya kumbakisha mshambuliaji wao, na wamefikia hatua hadi ya kutangaza jambo hilo hadharani.”

“Vardy ameamua yeye mwenyewe, na mimi sina budi kukubaliana na jambo hilo kwa sababu alikua anasubiriwa kutoa mustakabali wake.

“Japo tulitarajia angetoa jibu lake mapema, ila bado tunaheshimu maamuzi yaliyochukuliwa na Vardy ya kuendelea kubakia na klabu yake. Bado ana umri mdogo (miaka 29) na alichokiamua ni sahihi kwa mustabaki wa soka lake.”

Hata hivyo Wenger alisisitiza kuendelea na mpango wa kusaka mshambuliaji mwingine ambaye atajiunga na kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, ili kutimiza sehemu ya malengo aliyojiwekea.

Video: Mbunge anataka kulipwa Milioni 243 alizotumia kuchimba visima 9
Magufuli amtaka Kikwete atupe pembeni ya Gwajima na Ulimwengu