Hatimae meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amepasua ukweli wa mustakabali wa beki wa pembeni kutoka nchini Ufaransa Mathieu Debuchy.

Wenger amesema beki huyo aliyemsajili miaka mitatu iliyopita akitokea Newcastle Utd, hayupo katika mipango yake na huenda akamruhusu kuondoka itakapofika Januari 2017, wakati wa dirisha dogo la usajili.

Debuchy amekua na mazingira magumu ya kujumuishwa katika kikosi cha kwanza, tangu kinda kutoka nchini Hispania Hector Bellerin lilipoonyesha kiwango kilichomridhisha babu huyo, na kufikia hatua ya kumuweka kwenye mipango ya kikosi chake cha kwanza.

Suala la mustakabali wa Debuchy lilizungumzwa katika mkutano na waandishi wa habari, kufuatia taarifa za kuumia kwa Bellerin  ambaye atakua nje ya uwanja kwa muda wa majuma manne yajayo.

Waandishi wa habari walitaka kufahamu Wenger atamtumia mchezaji gani katika nafasi ya beki wa kulia kwenye mchezo wa kesho jumamosi dhidi ya Man Utd, ambapo alijibu swali hilo pasi na kumtaja Debuchy.

“Tuna wachezaji wengi ambao wana uwezo wa kucheza nafasi ya beki wa kulia kama Carl Jenkinson,”

“Pia tunaweza kumtumia Gabriel na Francis Coquelin ambao wana uwezo huo.

“Shkodran Mustafi naye anaweza kucheza nafasi ya beki wa pembeni, japo sipendi kuvuruga uhusiano wa mabaki wangu wa kati ambao kwa sasa unaendelea kukomaa.

“Hivyo ninatarajia kulifanyia kazi suala la beki wa kulia, na ninajua nani atacheza upande huo katika mchezo wa kesho dhidi ya Man utd.” Alisema Wenger.

Mathieu Debuchy alirejea Emirates Stadium wakati wa majira ya kiangazi, baada ya kumaliza mkataba wa mkopo na klabu ya Girondins de Bordeaux ya Ufaransa, ambayo ilimsajili mwanzoni mwa mwaka huu.

Mwanafunzi wa UDOM kizimbani kwa kufadhili magaidi wa Al-shabaab
Lionel Messi Apinga Agizo La Benchi La Ufundi FC Barcelona