Klabu ya Arsenal huenda ikafanya maamuzi ya kumtoa mshambuliaji wake Olivier Giroud kama sehemu ya kutimiza azma ya kumsajili Gonzalo Higuain wa SSC Napoli.

Mwandishi wa habari wa Italia Gianluca Di Marzio, ameandika katika tovuti yake kwamba, meneja wa Arsenal Arsene Wenger yu tayari kufanya maamuzi hayo kutokana na kuhitaji huduma ya mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina.

Di Marzio, amefafanua kuwa Wenger anaamini mtego wa kumpeleka Giroud SSC Napoli kama sehemu ya kumsajili Higuain utafanikiwa, kutokana na klabu hiyo ya mjini Naples kuhitaji mbadala wa mshambuliaji huyo ambaye imeshathibitika ataondoka katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.

Hata hivyo mwandishi huyo amesisitiza kwamba, huenda Wenger anaona ugumu wa kukubali kutoa kiasi cha Pauni milion 72 ambazo zimeshatajwa kama ada ya usajili wa Higuain, hivyo anataka kutumia njia ya mkato ili atimize lengo lake.

Rais wa SSC Napoli, Maurizio Sarri mwishoni mwa juma lililopita alikaririwa na vyombo vya habari akikiri kuwa shabiki mkubwa wa Giroud, ambaye alikuwa sehemu ya wachezaji walioanzishwa kwenye kikosi cha Ufaransa, ambacho kilishindwa kufurukuta mbele ya Ureno kwa kukubali kufungwa bao moja kwa sifuri.

Giroud mwenye umri wa miaka 29, aliifungia Arsenal mabao 21 msimu wa 2015-16, tofauti na Higuain ambaye alivunja na kujiwekea rekodi yake mwenyewe katika kikosi cha SSC Napoli kwa kupachika mabao 36 kwenye ligi ya nchini Italia (Serie A).

Video: Mabigwa wa Euro 2016 Walivyopokelewa Lisbon
Magazeti: Gwajima Alivyoingia kwenye 18 za Polisi, Wabunge Chadema Wapanga Kugoma