Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger amesema aliwahi kukataa kazi ya kukinoa kikosi cha mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris St-Germain, kutokana na mapenzi yake ya dhati yaliyojikita huko kaskazini mwa jijini London.

Wenger, mwenye umri wa miaka 66, amefichuia siri hiyo zikisalia saa kadhaa kabla ya kikosi chake hakijaanza kampeni ya kuwania ubingwa wa barani Ulaya msimu huu wa 2016/17 kwa kupambana na PSG mjini Paris.

Babu huyo ambaye mwaka huu atafikisha miaka 20 tangu alipoanza kukinoa kikosi cha Arsenal, amesema mwaka 2011, 2013 na 2014 aliwahi kufuatwa na viongozi wa PSG ili akatishe mkataba wake huko Emirates Stadium, lakini alikataa kufanya hivyo kutokana na mapenzi yake na The Gunners.

“Mara kadhaa nilijaribu kufikiria namna ya kukubali ofa yao, lakini iliniuwia vigumu kukubali kutokana na kuamini kwamba tayari klabu ya Arsenal imekua kama himaya yangu na ninaipenda kwa dhati.” Alisema Wenger alipozungumza na waandishi wa habari mjini Paris.

Katika hatua nyingine Wenger amesema mpambano wa hii leo utakua kipimo kizuri kwa kikosi chake kutokana na timu wanayokutana nayo kuwa katika kiwango cha juu katika ukanda wa barani Ulaya.

Amesema kipimo hicho anaamini kitatoa picha kamili ya utayari wa kikosi chake ambacho kwa msimu huu kimejipanga kupambana ili kumaliza kiu ya kufanya kutwaa ubingwa kwenye ligi ya nchini England na barani Ulaya.

PSG wanarejea katika michuano ya barani Ulaya, baada ya kutolewa katika hatua ya robo fainali msimu uliopita kwa kufungwa na Man City jumla ya mabao mawili kwa matatu.

Arsenal na PSG wapo katika kundi A sambamba na FC Basel ya nchini Uswiz pamoja na PFC Ludogorets Razgrad ya Bulgaria.

Guardiola Akataa Kupakwa Mafuta Kwa Mgongo Wa Chupa
Ni ajabu na kweli, Roboti afanya upasuaji wa macho kwa mara ya kwanza Uingereza