Aliyekua meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amesema anahitaji kupewa mtihani mgumu, baada ya kuondoka kaskazini mwa jijini London, ili kudhihirisha uwezo wake wa ukufunzi.

Wenger ametoa kauli hiyo, baada ya kukataa ofa kutoka kwenye klabu nguli duniani kama Real Madrid mara kadhaa, kwa kisingizio cha kuipenda Arsenal wakati akiwa mkuu wa benchi la ufundi la washika bunduki hao wa jijini London.

Meneja huyo mwenye umru wa miaka 68, tayari ameshathibitisha kuendelea kufanya shughuli za ukufunzi wa soka, baada ya kuondoka Arsenal majuma mawili yaliyopita.

Wenger amesema tangu alipoondoka Arsenal, amekua akipokea ofa nyingi tofauti na alivyotarajia, lakini bado hajaona uzito wa ofa hizo, kutokanana kuhitaji klabu ambayo itampa changamoto katika ukufunzi wake.

“Ninahitaji kupata mtihani mzito katika shughuli zangu za ukufunzi, ili nionyeshe ni vipi nipo tayari kupambana nao, baada ya kumaliza mtihani wa Arsenal kwa miaka 22,” amesema Wenger alipohojiwa na kituo cha televisheni cha BeIN Sports.

“Sijui nini kitatokea, lakini ninaendelea kusubiri ofa ambayo nitaona inanifaa, ili niweze kuitumikia tena taaluma yangu, kwa kufungua ukurasa mpya.”

Wenger pia akafafanua kwa nini aliwahi kukataa ofa za kujiunga na klabu ya Real Madrid, zaidi ya mara mbili alipokua mkuu wa benchi la ufundi la Arsenal.

“Ninafikiri ofa za Real Madrid zilitumwa kwangu zaidi ya mara mbili,” amesema.  “Real Madrid ni moja ya klabu kubwa duniani ninazozipenda, lakini sikuwa tayari kufanya kazi kwenye klabu hiyo, kwa sababu niliamini bado malengo yangu nikiwa na Arsenal Football Club, yalikua hayajatimia.

“Wakati ofa hizo zinakuja, nilikua kwenye mchakato wa kusaidia ujenzi wa uwanja wa Arsenal (Emirates stadium), kwa sababu mkopo uliochukuliwa kwa ajili ya ujenzi, dhamana iliwekwa kwa jina langu, hivyo ilikua vigumu kuondoka kwa wakati huo.”

Wenger ametoa kauli hiyo, ikiwa hii leo Zinedine Zidane ametangaza kujiuzulu nafasi ya umeneja ndani ya Real Madrid, na huenda ana makusudi ya kutaka aingizwe kwenye mchakato wa kumsaka mbadala wa mfaransa mwenzake huko Santiago Bernabeu.

Siwezi kuchambua tena masuala ya Katiba Mpya- Dkt. Bashiru
Zinedine Yazid Zidane ajiuzulu Real Madrid