Meneja wa klabu ya Arsenal Arsene Wenger, amesema kikosi chake kilikua na bahati ya ushindi katika mchezo wa jana, na ndio maana kiliibuka na point tatu muhimu kwa bao la dakika za mwisho lililofungwa na Laurent Koscielny.

Wenger ambaye alionekana kukata tamaa na suala la kupatikana kwa ushindi kwenye mchezo huo uliowakutanisha dhidi ya Burnley, alizungumza suala hilo la bahati mara baada ya kufanyiwa mahojiano na kituo cha televisheni cha SKY Sports.

Alisema ilikua ni bahati kwa Arsenal kupata ushindi wa bao moja, kutokana na hali ya mchezo ulivyokua, hivyo hana budi kuamini ilikua ni haki yao kuondoka katika uwanja wa ugenini wakiwa na point tatu mkononi.

Kuhusu madai ya Laurent Koscielny kushika mpira kama haujazama golini mwa Burnley, Wenger alisema hakuona kitendo hicho na aliahidi kutazama tena marudio ili kujiridhisha kama kweli beki huyo kutoka nchini Ufaransa aliunawa.

“Sikuona kama ameshika ama hakushika, itanilazimu kuangalia tena marudio ya mchezo huu ili nijiridhishe kama kweli Koscielny alifanya kitendo hicho.

“Hata kama nitabaini ni kweli ameshika bado ninaamini ni bahati kwetu kupata ushindi ambao umemfurahisha kila mmoja wetu hasa ikizingatiwa tulikua katika uwanja wa ugenini.” Alisema Wenger.

Katika hatua nyingine Wenger alikiri kutokufurahishwa na mfumo uliotumiwa na Burnley wa kukaa langoni wakati wote huku wakifanya mashambulizi ya kushtukiza.

Alisema jambo hilo liliharibu ladha ya mchezo, na wakati mwingine ilionekana kama wachezaji wake wapo katika mazoezi ya kuajiandaa na mchezo ambao walitakia kushambulia wakati wote.

“Haipendezi kwa timu kushindwa kucheza soka la ushindani, soka ni mchezo wa ushindani wakati wote, tunatakiwa kucheza kwa kushindana na kila mmoja kutumia nafasi anazozipata, lakini sio kwa aina ya mchezo ulioonyeshwa na wapinzani wetu wa kukaa langoni karibu dakika zote 90.” Alisema Wenger.

Ushindi wa bao moja kwa sifuri walioupata Arsenal katika mchezo wa jana, umewawezesha kufikisha point 16 ikiwa ni tofauti ya point mbili dhidi ya Man City walio kileleni wakifuatiwa na Spurs wenye point 17.

 

Samuel Eto'o Atoka Kifungoni
Zinedine Zidane: Hakuna Baya Linaloendelea Kikosini