Baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na mabingwa wa soka nchini Hispania FC Barcelona, kiungo kutoka Chile Arturo Vidal, amefunguka na kueleza matarajio yake akiwa Camp Nou.

Kiungo huyo aliyejiunga na FC Barcelona akitokea kwa mabingwa wa soka nchini Ujerumani FC Bayern Munich, amesema amefarijika kukamilisha ndoto zake za kucheza katika klabu hiyo kubwa duniani na yenye matamanio ya kufanya vizuri kila msimu.

Amesema mara kadhaa alikua na ndoto za kucheza sambamba na Lionel Messi, na aliitafuta nafasi hiyo kwa kipindi kirefu, na sasa hana budi kumshukuru mwenyezi mungu kwa kumjaalia kufanikisha mpango huo.

“Hii ilikua ndoto yangu ya siku nyingi, nimefanikisha nilichokihitaji kwa muda mrefu, sina budi kumshukuru mwenyezi mungu kwa kunikamilishia hili.

“Nitapambana vilivyo kwa kushirikiana na wenzangu, ninaamini mwishoni mwa msimu tutapata kitu, FC Barcelona kuna wachezaji wenye viwango vya hali ya juu, sina shaka na mafanikio ambayo yanategemewa na mashabiki wa klabu hiii.

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya mkataba wangu, ninatarajia mambo makubwa ambayo yataandika historia katika maisha yangu ya soka.

“Nina shauku kubwa ya kuanza kucheza sambamba na wachezaji kama Messi ambaye niliota usiku na mchana kucheza naye sambamba, Suarez, Sergio Busquet na wengine wengi.”

Vidal mwenye umri wa miaka 31 amejiunga na FC Barcelona kwa ada ya Pauni milioni 18 sawa na Euro milioni 20 (Dola za kimarekani milioni 23m), baadae hii leo (Jumatatu) nanatarajiwa kutambulishwa mbele ya mashabiki katika uwanja wa Camp Nou.

Usajili wake unatajwa kama mbadala wa kiungo kutoka nchini Brazil  Paulinho ambaye amerejea nchini China kwenye klabu ya Guangzhou Evergrande kwa mkopo.

Niko Kovac ampinga bosi wake FC Bayern Munich
Rachid Ghezzal kubebeshwa majukumu ya Mahrez

Comments

comments