Watu wawili wamepoteza maisha na wengine watano kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari mawili madogo, moja kutoka Tanzania na lingine kutoka nchini Kenya. Ajali hiyo imetokea Jumapili  ya Pasaka katika eneo la Oldonyosambu jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha (RPC), Jonathan Shanna amesema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa nyuma wakati magari hayo yakiongozana kwa kasi kujaribu kulipita gari la mbele yake bila kuchukua tahadhari.

“Ni kweli watu wawili wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari mawili aina ya Mitsubishi Saloon na Toyota. Ajali hiyo imetokea katika barabara ya Arusha Namanga majira ya saa tisa alasiri katika eneo la Oldonyosambu,” alisema Kamanda Shanna.

“Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari lililokuwa nyuma kutaka kulipita gari lililokuwa mbele yake iliyokuwa inakata kona kuelekea Ngalinanyuki, katika gari hilo watu wawili wamefariki ambapo mmoja ni Mtanzania anayejulikana kwa jina la Henry lakini jina lake lingine halijajulikana kwa sababu kitambulisho chake kimefutika-futika. Na mwingine aliyefariki ni Mkenya aliyekuwa dereva wa gari namba KCH 665 G Mitsubishi Saloon anayejulikana kwa majina ya Onesmo Mwangwi, umri wake miaka 20, ni Mkikuyu na mfanyabiashara,” aliongeza.

Kwa upande wa shuhuda mmoja ambaye ameeleza kuwa awali yeye alikuwa amepanga kwenye gari mojawapo lililopata ajali kabla ya kushuka ghafla na kuhamia kwenye gari lingine dakika chache kabla ya ajali hiyo, amesema kuwa hakukuwa na mashindano ya magari kama wengi wanavyoelezea bali ni vijana marafiki ambao hukutana nyakati za sikukuu na kufurahia pamoja wakichoma nyama.

“Mimi hata sikuwa na sababu ya kuhama kwenye hilo gari, nilijisikia tu kushuka nikahamia gari lingine. Baada ya muda mfupi gari nililohama likapata ajali na rafiki zangu wamepoteza maisha, wengine wamejeruhiwa,” Scort Edward aliwaambia waandishi wa habari.

Hakukuwa na mashindano, sisi vijana huwa tunakutana tu angalau mara mbili kwa mwaka tunapongezana, tunachoma nyama na kufurahi,” aliongeza.

Miili ya marehemu pamoja na majeruhi walikipelekwa katika hospitali ya Selian Lutheran.

Waumini wa Kanisa la Anglikani Njombe Waliombea Taifa misa ya Pasaka
Sudan: Waandamanaji wavutana kugawana madaraka, wavunja uhusiano na Jeshi