Na Nelson Kessy, Arusha

Mkutano wa 39 wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umeanza leo jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kukubaliana na ‘agenda’ mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo (Summit) utakaofanyika mwezi Februari, 2020.

Mkutano huo wa siku saba umeanza leo kwa ngazi ya maofisa waandamizi kutoka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na utafuatiwa na mkutano wa Makatibu Wakuu kisha kuhitimishwa na Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Jumuiya hiyo tarehe 27 na 28 Novemba, 2019.

Ajenda za mkutano huo zinakadiriwa kuwa tisa ambazo ni pamoja na ripoti ya utekelezaji wa maamuzi mbalimbali yaliyofikiwa na Baraza hilo kwenye vikao vilivyopita; taarifa kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, taarifa kuhusu masuala ya miundombinu, forodha na biashara; na ripoti ya kamati ya utawala na fedha.

Agenda nyingine ni taarifa ya Baraza kwa Wakuu wa Nchi kuhusu utekelezaji wa maamuzi/maelekezo mbalimbali yaliyotolewa kwenye mikutano ya Wakuu wa Nchi; na Kalenda ya Matukio ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kipindi cha kuishia mwezi Juni 2019.

 Jumuiya ya Afrika Mashariki inaundwa na nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Novemba 22, 2019
Breaking News: Waziri Mkuu wa Israel ashtakiwa kwa rushwa, udanganyifu