Hatimaye uongozi wa wa AS Roma umethibitisha kukamilisha dili la kumsajili mshambuliaji kinda kutoka nchini Uholanzi Justin Kluivert, akitokea Ajax Amsterdam kwa dau la Euro milioni 17.25.

AS Roma wamethibitisha taarifa za kumsajili Justin, kupitia tovuti ya klabu hiyo yenye maskani yake makuu mjini Roma nchini Italia, baada ya kuwa kimya kwa zaidi ya juma moja na nusu.

Justin, ambaye ni mtoto wa gwiji wa soka nchini Uholanzi Patrick Kluivet aliwasili mjini Roma majuma mawili yaliyopita kufanyiwa vipimo vya afya, lakini siku kadhaa baadae uongozi wa AS Roma ulikaa kimya, hatua ambayo ilihisiwa huenda dili la uhamisho wa mshambuliaji huyo limeyeyuka.

“AS Roma ina furaha kubwa kuwajulisha kwamba, Justin Kluivert amejiunga nasi kwa mkataba wa muda mrefu, baada ya kufanyiwa vipimo vya afya,” Imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti na AS Roma.

“Kluivert, mwenye umri wa miaka 19, amejiunga na klabu yetu akiwa mwenye furaha, tunaamini hali hiyo itaendelea na kuwezesha mipango tuliyojipangia kwa msimu ujao wa ligi ya Italia na michuano ya kimataifa.” Imeendelea kueleza taarifa hiyo.

Justin amesaini mkataba wa miaka mitano na uongozi wa AS Roma, ambao utamuweka Stadio Olimpico hadi mwaka 2023.

Mats Hummels kuwakosa Sweden
Video: Lembeli aivuruga CCM, Bashiru-Ruksa wabunge wa CCM kuikosoa Serikali