Klabu ya AS Roma, imeripotiwa kuwa katika mipango ya dhati ya kutaka kumsajili mlinda mlango kutoka nchini Poland pamoja na klabu ya Arsenal, Wojciech Szczesny.

AS Roma, wameripotiwa kuwa kwenye harakati hizo kufuatia uvumi unaoendelea unaomhusu mlinda mlango kutoka nchini Argentina, Sergio Romero ambaye huenda akajiunga na Man Utd akitokea Stadio Olympico.

Szczesny, anatajwa kuwa chaguo sahihi la kumrithi Romero, kutokana na umahiri wake aliouonyesha akiwa na klabu ya Arsenal, na inaaminika katika kipindi hiki itakua ni rahisi kumpa.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25, amekua na wakati mgumu wa kurejea langoni mwa Arsenal tangu mwishoni mwa mwaka 2014, baada ya kupata upinzani mkali kutoka kwa mlinda mlango kutoka nchini Colombia David Ospina.

Hata hivyo ujio wa mlinda mlango mahiri katika klabu ya Arsenal akitokea Chelsea, Petr ÄŒech, umeongeza hofu kwa kinda huyo kutokana na nafasi yake kuendelea kuwa shakani, hivyo inaaminika itakua rahisi kwa meneja wa Arsenal, Arsene Wenger kukubali kumuachia.

Kabla ya jina la Wojciech Szczesny kutajwa, AS Roma walikua na mipango ya kutaka kumrejesha nyumbani mlinda mlango wa klabu bingwa nchini Ufaransa PSG, Salvatore Sirigu lakini hali imeonekana kuwa ngumu zaidi kutokana na msimamo ulioonyeshwa na viongozi wa klabu hiyo ya jiji Paris.

Szczesny, tayari ameshaitumikia timu ya taifa ya Poland katika michezo 23.

Mrisho Mpoto Ahofia Upepo Wa ‘Timu Fulani’ Kumkosesha Ushindi AFRIMMA
Aliyemmwagia Fedha Bandia Blatter Kukiona Cha Moto