Serikali imezitaka asasi mbalimbali zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kuwa chachu ya maendeleo nchini ili kuweza kuhamasisha shughuli mbalimbali za maendeleo kwa vijana.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa kongamano la wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kwa lengo la kukuza uelewa katika kutekeleza programu ya kuwawezesha vijana kati ya Ujerumani na nchi za Afrika (African – German Youth Initiative).

Amesema kuwa Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya Taifa ya Ajira imekuwa ikihamasisha wadau mbalimbali kuanzisha Miradi na Programu zinazowawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kuweza kujiajiri au kuajiriwa katika Sekta mbalimbali ili waweze kuchangia kwenye maendeleo ya nchi.

“Vijana ndio chachu kubwa ya maendeleo endelevu, hivyo ni vyema wakatumia fursa zilizopo kuleta mabadiliko yatakayo kuwa na tija na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa.” amesisitiza Mhagama

Aidha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa vijana wanawezeshwa ipasavyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Beng’i Issa amesema kuwa Programu ya mabadilishano ya vijana (Exchange Program) imekuwa na manufaa makubwa sana katika kuwajengea uwezo vijana kupitia fani mbalimbali zinazoleta mabadiliko ya chanya katika Taifa.

Naye, Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC), Lenin Kazoba amesema kuwa kongamano hilo litakuwa na manufaa kwa vijana na asasi zinazoshughulikia maendeleo ya vijana kwa kuweza kujadili kwa pamoja fursa zitakazoleta maendeleo kwa vijana na jamii inayowazunguka.

Programu ya mabadilishano ya vijana kati ya Nchi ya Ujerumani na Tanzania ilizinduliwa rasmi tarehe 30 Juni, 2016 Mjini Bonn, Ujerumani na Waziri wa Uchumi wa Ushirikiano na Maendeleo Mhe. Gurd Muller ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa moja kati ya Nchi Tatu (3) Barani Afrika zilizopewa heshima kubwa ya kuchaguliwa kutekeleza mradi huo kwenye hatua ya majaribio kupitia Tanzania Youth Coalition (TYC). Zaidi ya vijana 4,015 wamefaidika kupitia program hiyo kwa kupata ujuzi na uzoefu wa fani mbalimbali.

Kidato cha kwanza waruhusiwa kuvaa sare za shule ya msingi
Video: Muswada huu wa sheria ni haramu kama nyama ya Nguruwe- Polepole