Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mfanyabiashara wa samaki aliyefahamika kwa jina la Nicholas Light (25) kwa tuhuma za kumuua mpenzi wake kwa kumnyonga hadi kufa wilayani Nyamagana.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi wakati akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amemtaja mwanamke aliyeuawa kuwa ni Victoria Swai (26) ambaye alikuwa akifanya kazi katika kampuni inayohusika na masuala ya anga.

Kamanda Msangi amesema kuwa chanzo cha mauaji hayo inasemekana ni wivu wa kimapenzi ambapo inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akimtuhumu marehemu kuwa anamsaliti kimapenzi, jambo ambalo lilisababisha kuzua ugomvi kati yao na kupelekea Nicholas kumnyonga mwanamke huyo kwa kumkaba shingo akiwa ofisini kwake na baadae kukosa pumzi hadi kufariki dunia.

Amesema kuwa mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa Bugando kwa ajili ya uchunguzi na pindi uchunguzi utakapokamilika utakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu ili waweze kufanya mazishi.

Kwa upande mwingine, Kamanda Msangi amewapa pole ndugu na familia kwa msiba walioupata pamoja na kutoa wito kwa wakazi wa jiji la Mwanza hususani vijana kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapokuwa kwenye migogoro.

Mbunge aomba muongozo baada ya kufinywa makalio
Mussa Mgosi: Simba ilistahili kushinda 6-0