Takribani watu milioni 828 sawa na asilimia 10 ya idadi ya watu duniani kote, wanalala njaa kila usiku na ikiwa ni asilimia 46 zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Takwimu hizo za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa – FAO, zinatoka katika ripoti yake ya karibuni imesema kati ya walioathiriwa na njaa, thuluthi mbili ni wanawake na asilimia 80 wanaishi katika maeneo yenye mabadiliko ya hali ya hewa.

Shirika lisilo la faida, la “The Hunger Project” liliitangaza tarehe 28 Mei kuwa Siku ya Kupambana na Njaa Duniani ili kuongeza ufahamu kuhusu viwango vya njaa ulimwenguni.

Njaa ni hali ya kudhoofisha mwili, ambayo hutokea wakati mwili unapokosa chakula kwa muda mrefu. Njaa ya muda mrefu inaweza kusababisha matatizo ya afya na inaweza kusababisha uharibifu wa kimwili kiakili na welewa hasa kati ya watoto wadogo.

Majanga na matatizo mbalimbali ya muongo mmoja, yamepelekea kupanda kiwango cha watu wenye njaa duniani katika miaka ya hivi karibuni. Kati ya 2019 na 2021, idadi ya watu wasio na lishe bora iliongezeka kwa zaidi ya milioni 150, ikichochewa na migogoro mbalimbali, mabadiliko ya hali ya hewa, majanga ya kiuchumi na janga la UVIKO-19 yaani corona.

Gharama ya maisha, imepanda na bei za chakula pia zimepaa. Kati ya 2019 na 2022, Fahirisi ya Bei ya Chakula ya FAO (FPI) – ambayo inapima mabadiliko ya bei ya kimataifa ya bidhaa za chakula ikiwa ni pamoja na sukari, nyama, nafaka, maziwa na mafuta ya mboga – iliongezeka kutoka pointi 95.1 hadi pointi 143.7.

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani (SOFI), iligundua kuwa idadi kubwa ya watu wasio na lishe bora duniani wanaishi barani Asia ambako takriban watu milioni 425 walikumbwa na njaa mwaka 2021. Lakini tunapoanglia kiwango cha njaa tutaona kuwa ni kikubwa zaidi barani Afrika, huku watu milioni 278 wakiathiriwa na njaa barani humo mwaka huo.

Wasimamizi miradi watakiwa kukamilisha kazi kwa wakati
TASAC yaelimisha jamii usafiri salama majini