Jeshi la polisi Zanzinzibar limemfukuza kazi askari polisi Hussein Yahaya Rashid (36) baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kusababisha kifo cha Mussa Suleiman ambaye alituhumiwa kwa kosa la wizi.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Awadh Juma Mohamed amethibitisha kufukuzwa kwa askari polisi huyo mwenye namba 3307412 ambaye mwezi Novemba mwaka jana alimkabidhi mtuhumiwa wa kosa la wizi kwa raia ambao walimshambulia hadi kusababisha kifo chake.

Kamanda Mohamed amesema askari huyo alitakiwa kumkabidhi mtuhumiwa kwa jeshi la polisi au kituo chochote kile ili kupata hifadhi na kusubiri taratibu nyingine za upelelezi pamoja na kufunguliwa mashtaka.

“Ni kweli Jeshi la polisi limemfukuza kazi aliyekuwa askari wake, Hussein Yahaya ambaye alimkamata raia anayetuhumiwa kwa makosa ya wizi, sasa yeye badala ya kumpeleka katika kituo cha polisi alimsalimisha kwa raia wenye hasira nakusababisha kifo chake” amefafanua kamanda Mohamed.

Na kuwataka askari wengine wa jeshi la polisi kuzifahamu sheria zinazoliongoza jeshi hilo ambalo linafanya kazi zake kwa ushirikiano mkubwa na raia.

“Jeshi la polisi kazi yake kubwa ni kulinda usalama wa raia, maisha yao na mali zao, huwezi kumkamata mtuhumiwa wa kosa la wizi na kumpeleka kwa raia wenye hasira na kumuua” amesisitiza kamanda Mohamed.

Barrick kupunguza wafanyakazi zaidi ya 100 North Mara
Mkutano wa Zitto wazuiliwa Kigoma