Picha ya askari polisi mwenye bunduki akiwa anaangalia usalama ndani ya chumba cha mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi nchini Kenya imezua gumzo zito.

Wanafunzi wa shule ya msingi wameendelea na mitihani yao ya kuhitimu, ambapo maafisa wanaoshughulikia elimu wamejaribu kuchukua hatua kukomesha wizi wa mitihani uliokuwa tatizo kubwa nchini humo.

Picha iliwekwa mtandaoni na ‘Nairobi News’ ilimuonesha askari polisi akiwa anaangalia usalama ndani ya chumba cha mitihani akiwa na bunduki mithiri ya mlinzi wa Benki Kuu, imewaamsha wazazi ambao wamedai kuwa hali hiyo inaweza kuleta taharuki kwa wanafunzi ndani ya chumba cha mitihani.

“Hata kwetu sisi watu wazima, ni taharuki isiyoelezeka kama ukijikuta umekaa kwenye chumba cha mtihani na mbele yako kuna afisa wa polisi mwenye bunduki, au hata kuwa kwenye chumba kimoja na askari,” Esther Njeri ambaye mwanaye anafanya mitihani hiyo amekaririwa na BBC.


Hata hivyo, Mkuu wa shule moja ya msingi jijini Nairobi, ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema suala la askari kuwa katika shule hizo sio tatizo na kwamba hawaingii ndani ya madarasa kama ilivyoelezwa.

“Suala la usalama kwenye vyumba vya mitihani ni muhimu na kuwa na askari wenye silaha sio hali mpya kwa kuzingatia kuwa hawaingii ndani ya vyumba vya mitihani… hii imefanyika kwenye shule nyingine kuhakikisha kuwa hakuna udanganyifu kwenye vyumba vya mitihani,” alisema.

Askari waliokuwa kwenye shule zinazofanya mitihani waliwaeleza waandishi wa habari kuwa wamepewa maelekezo ya kutomruhusu mtu yeyote kuingia kwenye eneo la shule.

Rais Uhuru Kenyatta alifanya ziara ya kushtukiza katika baadhi ya shule jijini Nairobi kuangalia mwenendo wa mitihani hiyo.

Video: QBoy Msafi aeleza alivyomalizana na WCB
Azizi kortini kwa mashtaka 75, adaiwa kunaswa na risasi 6,496