Askari Polisi aliyetajwa kwa jina la Daudi Masunga Elisha amemuua askari mwenzake, Petro Saimon Matiko kwa kumpiga risasi na kisha yeye kujiua jijini Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio  hilo katika eneo la Benki ya Posta eneo la Pamba wilayani Nyamagana jijini Mwanza japo chanzo cha tukio hilo bado hakijajulikana.

Kamanda Kamugisha alisema kuwa tukio hilo sio la kawaida kwa jeshi la Polisi na kwamba hali hiyo ilizua taharuki kubwa kwa wananchi waliokuwa katika maeneo hayo.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kamugisha alisema;

“Ni kweli kuna askari wawili wamefariki eneo la Benki ya Posta. Katika eneo la benki hiyo kulikuwa na askari wawili waliokuwa lindoni ambao ni PC Elisha na PC Remigius Alphonce mwenye namba H 4291, wakiwa wanaendelea na lindo alifika askari mwingine aliyekuwa amevaa kiraia PC Matiko na kuwasalimia kisha kuingia ndani ya benki kuchukua fedha.

“Baada ya dakika tano, Matiko alitoka nje na kuwaeleza askari wenzake kwamba mtandao unasumbua, wakati akieleza hivyo, ghafla askari PC Elisha aliweka chemba risasi ambapo mwenzake PC Alphonce alimhoji mbona unaweka risasi katika hali ya utayari wa kutumika na alijibiwa kwa ufupi kwamba ‘achana na mimi.’

“Ghafla alimfyatulia risasi PC Matiko na kumpiga eneo la bega la kushoto na kutokeza mgongoni na kuanguka chini, kitendo hicho kilimfanya PC Alphonce kukimbilia Benki ya Barclays ili kuomba msaada kwa askari wenzake waliokuwapo lindoni hapo.

“Kabla ya askari hao kufika, ilisikika sauti ya mlio wa risasi na baada ya kurudi alimkuta PC Elisha akiwa amejipiga risasi kwenye paji la uso na kutokea nyuma ya kisogo, tayari akiwa amepoteza maisha.”

Jumamosi ya mwisho wa mwezi Yatangazwa kuwa Siku Maalum ya Usafi
Rais Magufuli amalizia Safu ya Mawaziri wake, Awatangaza waliosalia