Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Medhodius Kilaini amezishangaa kauli zilizotolewa na Dk Wilbroad Slaa akiwatuhumu maaskofu wa kanisa hilo kupokea rushwa kutoka kwa mwanasiasa.

Akiongea jana mjini Bukoba, Askofu Kilaini ameeleza kuwa huenda Dk Slaa aliponyokwa na maneno yake kwa kuwa anafahamu dhahiri kwamba maaskofu wa kanisa hilo hawanunuliki bali hupokea michango kwa kazi mbalimbali za kanisa.

“Kwa kweli hii kauli inasikitisha, nisingetegemea Dk Slaa angetoa kauli kama hiyo kwa sababu alikuwa katibu mkuu wa baraza la maaskofu na mimi ndiye niliyechukua nafasi baada yake na anajua kanisa linavyofanya kazi,” alisema Askofu Kilaini.

“Kanisa linachangisha, hata na yeye wakati wa ujio wa Baba Mtakatifu alikuwa anachangisha wanasiasa na kila mmoja. Na hao wanasiasa wanachangia, Lowassa vilevile ni mchangiaji mzuri sana katika hafla za kanisa lakini hata siku moja hauwezi kusema kwamba kwa sababu mtu fulani amechangia, amekununua, maaskofu wa katoliki hawanunuliki” alisisitiza Askofu Kilaini.

Aliongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa vyama vingi nchini, Kanisa Katoliki liliamua kutojihusisha na masuala ya kisiasa na kwamba wapo kwa ajili ya kuiombea amani nchi yetu.

Alitoa mfano wa mwaka 2010 ambapo viongozi wa dini kwa pamoja waliungana kuliombea taifa bila kujali tofauti za kiimani, kutokana na vurugu zilizojitokeza visiwani Zanzibar.

Aliwataka wanasiasa wote kutoa dini kama kigezo cha ushawishi katika harakati zao za uchaguzi. Askofu huyo pia aliwataka wanasiasa kutotumia matusi na vyombo vya dola kutotumia nguvu bila sababu za msingi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye ambaye alishambuliwa na Dk Slaa, amesema kuwa hatapoteza muda wa kujibu alichokisema bali atasonga mbele na kujikita na kampeni za Chadema na Ukawa.

JK amshangaa Tena Sumaye
Berbatov Akabidhiwa Jezi Namba 10 PAOK Salonika